Na Zainab Nyamka,Blogu ya Jamii.
UONGOZI wa Yanga umesema hawawezi kupangiwa tarehe ya Uchaguzi na Shirikisho la Mpira wa miguu (TFF) na tayari wameshapanga tarehe ambapo kwa sasa utafanyika Juni 11 badala ya ile ya awali Juni 25.Uamuzi huo umekuja baada ya kukutana kwa kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo pamoja na bodi ya wadhamini. Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho hilo ilipewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa Yanga na Baraza la Michezo la Taifa(BMT).
TFF ilishaanza mchakato wa utoaji fomu kwa wanachama wa klabu hiyo na hadi juzi wagombea tisa wameshajitokeza kuchukua na kurudisha fomu kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali. Akizungumza juu ya mabadiliko ya uchaguzi ya klabu hiyo Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedit amesema kuwa wao kama klabu wameamua kupanga tarehe wanayohisi itawafaa. Uongozi wa Yanga ulishtushwa na agizo la TFF kusimamia uchaguzi wao bali suala hilo lilizua pia maswali mengi kutoka kwa wanachama wa klanbu hiyo.
Amesema wanachama hao walishangazwa na kitendo cha Serikali kuitaka TFF kusimamia uchaguzi huo wakati wao kama klabu wana kamati ya uchaguzi. Baraka amesema kuwa kitu cha ajabu zaidi ni TFF kutoa fomu hizo bila kuwasiliana nao ili kujua kma wanaochukua fomu hizo ni wanachama halali na kama wana Yanga wameamua kuja na msimamo wao na kupanga tarehe za mchakato mzima wa uchukuaji fomu hadi kutangaza matokeo.
Klabu imepanga ratiba yake ambapo June 2 na 3 itakuwa siku ya kuchukua fomu na kurejesha huku June 4 ikiwa ni siku ya mchujo wa awali na kubandika orodha ya wale waliopita, June 5 itakuwa ni siku ya mapingamizi huku June 6 na 7 ikiwa ni siku ya kupitia mapingamizi, kufanya usaili wa awali na kupeleka majina ya waliopita TFF. June 7 hadi 10 itakuwa ni siku ya wagombea kufanya kampeni kuelekea siku ya uchaguzi ambayo ni June 11 huku matokeo yakitangazwa siku Juni 12. Alisema uchaguzi huo utatumia katiba yao ya mwaka 2010 huku wanachama wakiruhusiwa kutumia kadi walizonazo zikiwemo zile za Posta Bank pamoja na CRDB.
"Tunapenda wanachama wetu kufahamu kuwa kadi zote zitatumika kupiga kura hivyo wasiwe na wasiwasi kikubwa wawe wamelipia kadi zao za uanachama licha ya kutumia katiba ya 2010", amesema Baraka. Akitolea ufafanuzi juu ya fomu za awali zinazotolewa na TFF, baraka amesema kuwa watafanya utaratibu kwa kushirikiana na TFF kwani hawana hakika kama kweli ni wanachama au laa. Baraka amesema, pia wanashangazwa na kauli za viongozi wa TFF kusema kuwa hawautambua uongozi uliopo madarakani wakati majina ya viongozi wa klabu hiyo yapo. "Kama ni kweli hawatambui uongozi wetu mbona barua zao zinapitia kwa mwenyekiti na katika makombe yetu tuliyoshinda pongezi zilienda kwa mwenyekiti, iweje leo waseme hawatambui uongozi uliopo?", amesma Baraka.
Wakati huo huo.
YANGA YAWASHUTUMU VIGOGO WA SERIKALI NA TFF KUHUJUMU UCHAGUZI WAO.
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema umebaini mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya watu ili kutaka kuvuruga uchaguzi wao na lawama hizo zimetupwa moja kwa moja kwa baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, viongozi wa Serikali pamoja na watendaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF). Yanga si wa kwanza kutupa lawama kwa TFF kwani ni juzi tu kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) alielekeza lawama zake kwa mmoja wa watendaji wa TFF.
Kinacholalamikiwa zaidi kwa mtendaji huyo ni kuchelewesha kwa makusudi zoezi zima la uchukuaji fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali. Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo, Afisa habari wa Yanga, Jerry Muro alisema kuwa wanashangazwa na kitendo cha baadhi wa watendaji hao kutaka kuwahujumu ila kwa bahati mbaya hujuma hizo zimegonga mwamba kwani uchaguzi wao utafanyika na tayari wana ushahidi wa kutosha juu ya watu hao.
Jerry amesema kuwa tayari wana ushahidi wa sauti na video unaoonesha mipango ya kuharibu uchaguzi wa klabu yao. "Tunawajua watu wanaotaka kuvuruga klabu yetu na tuna ushahidi wa sauti na video unaoonesha vile vyote walivyokuwa wanavipanga", amesema Muro. Kinachosubiriwa sasa ni kuukamilisha ushahidi huo na kuuweka hadharani ili watu wabaini hujuma wanazofanyiwa.
Muro amewataka watu hao wasithubutu kuendelea kuingia uchaguzi wao na endapo wataendelea na vitendo hivyo wataonja joto ya jiwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...