Wajumbe wa Kamati ya Fedha Halmashauri ya Mji Njombe wakipata
ufafanuzi juu ya ujenzi wa stand mpya ya Mabasi inayofadhiiliwa na
Benki ya Dunia kupitia Mradi wa kukuza na kuendeleza Miji (ULGSP),
mradi ambao unatekelezwa kwenye Halmashauri 18 Nchini.
Ujenzi wa Jengo la vyumba 04 vya madarasa unaoendelea katika Shule ya
Sekondari Mgola.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha Halmashauri ya Mji Njombe wakiwa wamesimama
Nje ya jengo la zahanati ya Utalingolo iliyopo katika Kijiji cha
Utalingolo ambayo ipo katika hatua za umaliziaji. Wa kwanza kulia ni
Mwandisi wa Halmashauri Eng. Ibrahim Mkangalla.
Na Hyasinta Kissima - Njombe
Halmashauri ya Mji Njombe imetoa jumla ya shilingi milioni 128 kwa mwaka wa fedha 2015/2016
ili kukamilisha ujenzi wa zahanati na ununuzi wa vifaa vya zahanati kwenye jumla ya zahanati 12
zilizopo kwenye Halmashauri hiyo.
Akitoa ufafanuzi kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofanywa na Kamati ya fedha ya
Halmashauri, Mchumi wa Mji Njombe Ndugu Shigela Ganja amesema kuwa fedha hizo zilitolewa
ziliambatana na maelezo ya kuhakikisha kuwa zinamalizia shughuli za ujenzi ili kuhakikisha kuwa
zahanati hizo zinaanza kutoa huduma kwa wananchi haraka iwezekanavyo na kupunguza adha ya
Wananchi hususani waliopo maeneo ya Vijijini ambapo huduma za afya zimekuwa ni za tabu.
Akifanya majumuisho ya ukaguzi wa miradi kwa upande wa Zahanati, Mwenyekiti wa Halmashauri
Mheshimiwa Mwanzinga amesema kuwa miongoni mwa Zahanati ambazo Kamati yake imezikagua
zinaridhisha ingawaje usimamizi wa karibu zaidi unahitajika ili kuhakikisha fedha ambazo
halmashauri imezipeleka zinatumika kwa mujibu wa maelekezo na zinakamilika kwa wakati.
“Lengo la kuzisimamia Zahanati hizo ni kuhakikisha kuwa mpaka kufikia mwaka 2017 Majengo
yote ya zahanati zilizokwisha patiwa fedha zinaanza kutoa huduma kwa Wananchi kama tulivyoahidi
katika Kampeni za uchaguzi. Kuna Kata ambazo licha ya Zahanati zake kupatiwa fedha na
Halmashauri tangu mwezi Mei mpaka sasa, fedha hizo bado zipo kwenye Akaunti na Diwani wa kata
husika yupo kimya. Zahanati hizo zinakuwa kero si kwa Kamati yangu bali hata kwa wale
wananchi wa maeneo husika kwani zinakuwa za muda mrefu na bado ujenzi wake unakua hauna
matumaini kwa Wananchi wa eneo husika.
Nawataka Waheshimiwa Madiwani washirikiane na
Wataalamu katika usimamizi wa Zahanati hizo”
Aidha Mwanzinga ameitaka Halmashauri kuwaandikia madiwani wasiofahamu majukumu yao barua
ya kuwakumbusha majukumu yao ya kazi kwani moja kati ya jukumu la diwani ni kufanya
usimamizi wa miradi inayoendelea ndani ya Kata yake na kuitolea taarifa kwenye vikao mbalimbali
vya Kisheria pale panapokuwa na changamoto inayokwamisha mradi husika kutokabidhiwa kwa
Wananchi kwa wakati.
Nae mjumbe wa Kamati ya fedha wa Halmashauri Filoteus Mligo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya
Lugenge amesema kuwa ni vyema Halmashauri itoe vipaumbele vya zabuni kwa wakandarasi ambao
wanamaliza kazi zao kwa ubora na kwa wakati ili kuhakikisha kuwa miradi ya Halmashauri
inakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mligo ameongezea kuwa ni jukumu la Waheshimiwa Madiwani kuhakikisha
wanawahamasisha wananchi wa Kata zao kuendelea kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ili
miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati badala ya kuitegemea serikali pekee.
Miradi mingine iliyotembelewa na Kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa madarasa, ujenzi wa stand
mpya ya mabasi, ujenzi wa vyoo na ujenzi wa nyumba za kulala waalimu katika shule za sekondari.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...