Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera akizungumza juzi na wananchi wa Kijiji cha Duru, Tarafa ya Goroa Wilaya ya Babati juu ya wao kujiunga na mfuko wa afya ya jamii iliyoboreshwa (CHF).
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera amewaagiza viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Babati kuhakikisha hadi Desemba mwaka huu kaya 40,642 zinajiunga na mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa (CHF) hivyo kufikia asilimia 50 ya kaya za wilaya hiyo.

Akizungumza kwenye kata ya Duru Tarafa ya Goroa, Dk Bendera alisema wilaya hiyo ina kaya 81,284 hivyo viongozi wa wilaya hiyo wahakikishe hadi mwezi Desemba wawe wamefanikisha nusu ya kaya zijiunge na mfuko huo.

Dk  Bendera alisema suala la kupatiwa matibabu pindi mtu akiugua halina mjadala hivyo viongozi wa ngazi tofauti kwenye wilaya hiyo wanapaswa kufuatilia ili kaya hizo zijiunge na mfuko huo ambao una manufaa kwao.

Alisema viongozi wote wa eneo hilo wanapaswa kuhakikisha jamii inajiunga na mfuko huo kwani ni ukombozi wao kwenye sekta ya afya na siku wakistaafu wananchi watawakumbuka kwa kusababisha mabadiliko ya huduma hizo.

“Naibu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla alitoa agizo kwa mkoa wa Manyara kuhakikisha baada ya miezi sita ijayo tufikie asilimia 50 ya kaya zote kujiunga na CHF iliyoboreshwa,” alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati Hamis Malinga akizungumza mbele ya Dk Bendera, alisema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wananchi wa eneo hilo wanajiunga kwa wingi na mfuko huo.

Malinga alisema kupitia timu waliyonayo kuanzia ngazi ya vijiji, kata na tarafa, watatimiza majukumu yao kwa kupeana mrejesho kila mwezi ili kutambua wamefikia hatua gani na wanatarajia hadi mwezi Desemba watafanikisha.

Meneja wa mfuko wa Taifa wa bima ya afya nchini (NHIF) mkoani Manyara, Isaya Shekifu alisema mpango wa CHF ulioboreshwa utawawezesha kila kaya ya watu sita baba, mama na watoto wanne ambao hawajafikisha miaka 18 kupata matibabu kwa gharama ya sh30,000 katika mwaka mzima.

Shekifu alisema bima ya afya ni muhimu kwa sababu siyo kila mtu anapopata ugonjwa ana uwezo wa kugharamia matibabu na nchi zilizoendelea zimefanikiwa kupunguza vifo visivyo na lazima kwa kuhakikisha watu wanajiunga na mfuko.

“Katika CHF ya zamani huduma za nje tu ndizo zilizotolewa, hii iliyoboreshwa huduma ya magonjwa ya nje, kulazwa, upasuaji na vipimo ikiwemo x- ray zinatolewa kwa wanachama waliojiunga bila kulipia,” alisema Shekifu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...