Michuano ya kimataifa ya kirafiki (ICC) inaendelea katika nchi za China, Marekani na Australia, na alfajiri ya leo ilipigwa michezo mitatu iliyofanyika nchini Marekani.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika dimba la Sports Moles, Columbus kikosi cha Paris St-Germain chini ya kocha mpya Unai Emery kilitoa kipigo cha mbwa mwizi kwa vijana wa Real Madrid chini ya kocha Zinedine Zidane cha mabao 3-1.

PSG waliandika bao la kwanza dakika ya kwanza ya mchezo lililofungwa na Ikone baada ya kuwapiga chenga walinzi kadhaa wa Madrid na kufunga bao. Madrid walijaribu kusawazisha bao hilo lakini walijikuta wakipachikwa bao la pili kunako dakika ya 24,bao ambalo lilipachikwa na mchezaji Meunier kwa shuti kali la umbali wa mita 25.

Madrid walionekana kuchanganyikiwa zaidi na kuwapa nafasi PSGkuweza kutawala mchezo na kufanikiwa kufunga goli la 3 kupitia tena kwa mchezaji Meunier kunako dakika ya 39 ya mchezo baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Madrid ambao aliupiga yeye mwenyewe mfungaji wa bao hilo.

Madrid walijipatia bao la kufutia machozi katika dakika ya 43 kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Marcelo. Penati hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya mchezaji Aurier wa PSG kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika mabao yalikuwa hayo 3-1, na zaidi ya hayo kipindi cha pili nacho kiliisha bila ya bao lolote kupatikana.
Kwenye dimba la Soldier Field Stadium jijini Chicago, mpambano mkali wa kukata na shoka ulipigwa kati ya Ac Milan ya Italia na Bayern Munich ya Ujerumani.Katika mpambano huo timu hizo zilitoka sare ya kufungana mabao 3-3.

Walikuwa ni Ac Milan waliohanikiza bao la kwanza kupitia kwa mchezaji M'baye Niang akimalizia kwa ustadi kampa kampa tena ya wachezaji wenzakedhidi ya ya wachezaji wa Bayern. Frank Ribery akitumia uzoefu wake aliisawazishia Bayern Munich bao na muda mfupi baadaye David Alaba akaifungia Bayern bao la pili.Hadi mapumziko Bayern 2, Ac Milan 1.

Kipindi cha pili Milan waliingia na nguvu mpya na kuweza kusawazisha goli lililofungwa na Andrea Bertolacci.Kabla Bayern hawajakaa vizuri wakapachikwa goli la 3 lililofungwa na Kuck. Watu wakiamini Bayern wamelala,wakafanya shambulizi hatari lililopelekea mchezaji wao kufanyiwa madhambi ndani ya sanduku la hatari na mwamuzi akaamuru mkwaju wa penati upigwe, ambapo bila ajizi Ribery akaukwamisha mpira wavuni na kufanya ubao wa matangazo usomeke 3-3.

Katika kupigiana mikwaju ya penati Ac Milan wakapata penati zote 5 ambapo Bayern Munich wakaambulia penati 3,na Ac Milan kuibuka washindi wa mchezo huo.

Goli la dakika ya 4 tu ya mchezo lililofungwa na mlinzi wa Chelsea Gary Cahill kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Fabregas lilitosha kudumu mpaka mwisho wa mchezo na kuipa ushindi timu hiyo dhidi ya Liverpool.

Mtanange huo ulipigwa katika dimba la Rose Bowl,Pasadena huko Calfornia ulitawaliwa zaidi na Liverpool kiasi cha asilimia 65 kwa 35 za Chelsea. Kocha Antonio Conte wa Chelsea alitumia muda mrefu kuwahamisa wachezaji wake wajilinde zaidi (kupaki basi) na kuwapa Liverpool muda mrefu wa kulishambulia lango la Chelsea na kufanikiwa kufunga goli lililofungwa na Roberto Filmino lakini kwa mshangao wa wengi mwamuzi wa pambano hilo alilikataa kwa madai kuwa mfungaji alikuwa ameotea.


Katikati ya kipindi cha pili mwamuzi alilazimika kumpa kadi nyekundu ya moja kwa moja kiungo wa Chelsea Fabregas kwa kumchezea rafu mbaya mchezaji mpya wa Liverpool mlinzi Klavan, ambaye aliendelea na mchezo baada ya kupatiwa matibabu. Mpaka mwisho wa mchezo Chelsea waliibuka na ushindiwa goli 1-0.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...