Bodi ya filamu Tanzania imeahidi kuendeleza ushirikiano na wadau
wa sekta ya filamu kuhakikisha sekta hiyo inakuwa chachu ya maendeleo nchini.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa bodi hiyo Joyce
Fissoo wakati akifungua mafunzo ya uandishi wa miswada ya picha jongefu kwenye
ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO leo jijini Dar-es-salaam.
Mafunzo hayo ya siku nne yamewezeshwa kwa ushirikiano kati ya
Bodi ya Filamu Tanzania na Chama cha Waandishi wa Miswada ya Picha Jongefu
Tanzania (TASA).
Kwenye hotuba yake Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo alisisitiza
umuhimu wa mswada kwenye utengenezaji wa filamu pale aliposema “mswada ni
msingi wa filamu yoyote na mswada bora ndio utakao kuhakikishia filamu bora”.
Aidha ameupongeza uongozi wa Chama wa Waandishi wa Miswada ya
Filamu Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo ambapo ameonyesha imani yataleta
mabadiliko chanya kwenye ubora wa filamu za ndani. Mbali na kuwapongeza
viongozi wa chama hicho pia aliahidi kutoa ushirikiano wakati wowote
atakapohitajika ili kuboresha tasnia ya filamu ncini. Kutekeleza kwa vitendo
ahadi hiyo Fissoo alikubali kuwalipia ada ya uanchama washiriki wanane ambao
walikuwa bado hawajajisajili kwenye chama hicho.
Mafunzo hayo ya siku nne yatakuwa ya vitendo na shirikishi
ambapo yataongozwa na wakufunzi wawili kutoka nchini Marekani na yana lengo la
kuwaongezea ujuzi waandishi wa miswada ya filamu wapatao 65 ili waweze kuandika
miswada yenye ubora wa kimataifa.
Takwimu za Bodi ya Filamu Tanzania zinaonyesha jumla ya miswada
33 iliwasilishwa mwaka wa fedha 2014/2015 kati ya jumla ya filamu zaidi ya 1400
zilizokaguliwa. Idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na maombi 169
yaliyowasilishwa ndani ya mwaka huo kutoka kampuni za nje ambapo mamombi yote
sawa na asilimia 100 yaliambatanishwa na miswada yake.
Kwenye risala yake Katibu wa TASA Christian Kauzeni alizitaja
baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo wanachama wao ni pamoja ukosefu wa sera
ya filamu, wanachama kushindwa kujua wajibu wa mamlaka zinazosimamia sekta ya
filamu kama vile COSOTA, Bodi ya Filamu Tanzania, Baraza la Sanaa Tanzania
(BASATA)na kukosekana kwa mfumo yakinifu wa elimu kwa waandishi wa miswada ya
filamu. Bi. Fissoo aliahidi kuzishughulikia changamoto hizo.
Imetolewa
na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano
Bodi
ya Filamu Tamnzania
Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya Waandishi wa Miswada ya Filamu kwa baadhi ya waandishi
hao leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha
Waandishi wa Miswada ya Filamu Tanzania (TASA) Haji Jumbe.
Mwandishi wa Script kutoka Marekani Bi. Emma
Rosenbaum akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uandishi wa Miswada ya Filamu kwa baadhi ya waandishi
hao leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo na
Mwanafunzi wa Utengenezaji wa Filamu kutoka Los Angels Marekani Leo
Masciarelli.
Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Miswada ya
Filamu Tanzania(TASA) Bw. Christian
Kauzeni akisoma risala ya Chama hicho wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya
Waandishi wa Miswada ya Filamu kwa baadhi ya waandishi hao leo Jijini Dar es
Salaam.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi.
Joyce Fissoo akipeana mkono na Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Miswada ya
Filamu Tanzania (TASA) Cheristian Kauzeni mara baada ya kukabidhiwa fomu kwa ajili ya
kujiunga na chama hicho leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya waandishi wa Miswada ya Filamu wakifuatilia mafunzo ya Uandishi wa Miswada
kutoka kwa Mwandishi Mtaalam kutoka Marekani leo Jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...