Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), kujenga chelezo (gereji ya
kukarabati meli na vivuko), katika bandari ya Dar es Salaam ili kuokoa fedha nyingi
zinazotumika kwa matengenezo nje ya nchi.
Waziri Prof. Mbarawa amesema hayo wilayani Kyela, wakati alipokuwa akikagua
maendeleo ya ujenzi wa meli mbili mpya za mizigo zinazojengwa na Kampuni ya
Songoro Marine katika bandari ya Itungi ambayo ni Bandari Kuu katika Ziwa Nyasa na
kuelezea kuridhishwa kwake na hatua za ujenzi uliofikiwa.
“Tukijenga chelezo Dar es Salaam tutaokoa fedha nyingi tunazozipeleka nje kila mwaka
kwa ajili ya ukarabati wa vivuko na meli zetu", amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amesisitiza kuwa kujengwa kwa chelezo katika bandari hiyo kutaongeza ajira kwa
wananchi na pato kwa mamlaka kwani vyombo vya Sekta binafsi vitaweza kufanyiwa
ukarabati wa vyombo vyao vya majini.
Aidha katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara
ya Kikusya-Ipinda- Matema KM 34.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami na kumtaka
Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kukamilisha kwa viwango na ubora unaotakiwa
ili idumu kwa muda mrefu.
"Tunapotoa fedha tumedhamiria kuhakikisha kitu tunachofanya kiendane na thamani ya
fedha hiyo hivyo hakikisha unatekeleza kazi hii kwa kuzingatia viwango na ubora
unaotakiwa",amesisitiza Prof.Mbarawa.
Hata hivyo Prof. Mbarawa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi
anayejenga barabara hiyo ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa haraka na kufungua
uchumi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa
Mbeya Eng. Paul Lyakurwa amemuomba Waziri Mbarawa kuruhusu
wahandisi wazalendo kuendelea kusimamia mradi huo ikiwa ni hatua ya kuwajengea
uwezo watanzania kusimamia miradi mikubwa nchini.
Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu na kuongea na
wafanyakazi waliopo chini ya wizara yake katika mkoa wa Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akielekea
katika Bandari ya Itungi kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli mbili mpya zinazojengwa
katika bandari hiyo wilayani Kyela.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Eng. Salehe Songoro akitoa maelezo ya hatua
iliyofikiwa katika ujenzi wa meli mbili mpya mbili kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea bandari ya Itungi kuona
maendeleo ya ujenzi huo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua
jambo kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Eng. Salehe Songoro wakati
alipokagua moja ya mashine ya meli mpya inayojengwa katika bandari ya Itungi,
wilayani Kyela.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto),
akikagua risiti za malipo na Mhasibu wa Bandari ya Itungi (wa pili kushoto), wilayani
Kyela.
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...