Na: Lilian Lundo - MAELEZO
Tume ya Vyuo
Vikuu Tanzania (TCU) imeongeza muda wa udahili wa wanafunzi wanaotarajia
kujiunga na vyuo vikuu mwaka wa masomo 2016/2017 ili kuwapa fursa waombaji ambao wana sifa lakini hawakupata
vyuo kutokana na ushindani wa vyuo na kozi walizozichagua.
Hayo
yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Eleuther Mwageni alipokuwa akiongea
na waandishi wa habari juu ya mwenendo mzima wa udahili kwa mwaka wa masomo
2016/2017, leo Jijini, Dar es Salaam.
“ Tume imekamilisha
awamu ya kwanza ya udahili kwa waombaji wenye sifa ya kidato cha 6, ambapo
jumla ya waombaji wote ilikuwa 55,347, waombaji wenye sifa ni 47,203 sawa na
asilimia 85.3 ya waombaji wote. Katika waombaji hao wenye sifa waliopata vyuo
ni 30,731 sawa na asilimia 65 na waombaji 16,472 ambao wana sifa sawa na
asilimia 35 hawajapata vyuo hadi sasa, waombaji waliokosa sifa ni 8,144,”
alifafanua Prof. Mwageni.
Amesema kuwa
Tume imeamua kuongeza muda wa udahili kuanzia Septemba 12 mpaka Septemba 23,
2016 ili kuwapa nafasi waombaji wenye sifa, fursa ya kuomba tena vyuo na kozi
zenye nafasi kutokana na wengi wao kuomba
vyuo na kozi za aina moja.
Prof.
Mwageni alivitaja vyuo ambavyo vimeombwa na waombaji wengi na tayari vimeshajaa
kuwa ni Chuo cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kikatoliki
cha Afya na Sayansi Shirikishi, Chuo Kikuu cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro(KCMUCo)
na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.
Pia
alizitaja kozi ambazo zimechaguliwa na waombaji wengi kuliko nafasi zilizopo
kuwa ni kozi ya Ualimu, Udaktari wa Binadamu, Ufamasia, Uhandisi, Sayansi ya
Uthamini wa Ardhi na Sheria. Alitoa mfano wa kozi ya Ualimu Chuo Kikuu
Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam ilikuwa na waombaji 15,803 wakati nafasi ni
1,000.
Hivyo
amewashauri waombaji waliokosa nafasi kuomba vyuo na kozi zisizo na ushindani
ili waweze kupata nafasi kwa awamu hii ya pili.
Aidha Tume
hiyo imepunguza viwango vya udahili kwa waombaji wenye sifa ya stashahada
kutoka GPA 3.5 mpaka 3.0. Hivyo wamewataka waombaji wenye vigezo hivyo kuomba
vyuo na kwa wale waliomba awamu ya kwanza hawatatakiwa kuomba tena bali
kusubiri matokeo ya waombaji wenye sifa ya stashahada.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...