Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema utamaduni wa kupima afya kila baada ya kipindi ni jambo la
msingi linalomuwezesha Mwanaadamu kuendelea kuishi vizuri kwa matumaini.
Alisema vipo baadhi ya vifo vya kushitua
vinavyowashangaza watu katika maeneo mbali mbali lakini vikichunguzwa chanzo
chake hubainika kuwa ni ukosefu wa utambuzi wa maradhi yaliyokuwa
yakimsumbua marehemu ambayo wataalamu walikuwa na uwezo wa kuyatibu.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa
Jimbo la Mahonda alisema hayo wakati akizindua rasmi Kambi ya Siku
mbili ya Uchunguzi wa maradhi mbali mbali yanayowasumbua wananchi pamoja na
kutolewa dawa bure, miwani za kusomea kwa wale watakaobanika kuwa na matatizo
ikiwemo pia operesheni za Macho.
Kambi hiyo iliyofunguliwa katika Kituo cha Afya
Mahonda inaendeshwa chini ya udhamini wa Jumuiya ya Kimataifa ya kuhudumia
jamii ya Baps Charities ikijumuisha wataalamu na Madaktari Bingwa wapatao
kumi kutoka Nchini India na Dar es salaam.
Balozi Seif aliwaeleza wananchi hao waliojitokeza
kufanya uchunguzi wa Afya zao kuwa na tahadhari ya kujiepusha na ongezeko la
maradhi ya kisukari na shindikizo la Damu kwa kuwaona wataalamu wa afya pale
wanaoanza kuona dalili za maradhi hayo.
Alisema vifo vingi vinavyotokea ndani ya
jamii kwa sasa vinaripotiwa kuhusisha maradhi ya Kisukari na sindikizo
la Damu ambayo hatimae mgonjwa anaishia kukumbwa na maradhi ya kiharusi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza na
kuishukuru Jumuiya hiyo ya Kimataifa ya kuhudumia Jamii ya Baps Charities kwa
mchango wake mkubwa wa kusaidia jamii yenye kipato cha chini na mazingira
magumu.
Mapema Mweka Hazina wa Jumuiya ya Baps Charities
Bwana Kapil Dave alisema Taasisi yao imeamua kutoa huduma za Afya kwa jamii
ya kipato cha chini baada ya kubaini ongezeko kubwa la gharama katika
upatikanaji wa huduma za afya.
Bwana Kapil aliwatoa hofu Wananchi kwamba huduma
za Afya pamoja na Dawa zinazotolewa na Wataalamu na Mabingwa wa Taasisi hiyo
hazina mashaka yoyote baada ya kufanyiwa uhakiki na vyombo vinavyohusika
Kimataifa.
Mweka Hazina huyo wa Jumuiya ya Baps Charities
aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na watendaji wote wa
Sekta ya Afya waliochangia kuwajengea mazingira bora ya uchunguzi pamoja na
utowaji wa huduma za Afya hapa Zanzibar.
Bwana Kapil alifahamisha kwamba ushirikiano huo
wa pande mbili ndio uliowawezesha wataalamu wa Afya wa Baps kurejea kutoa
huduma tena Zanzibar baada ile huduma waliyotowa mwanzo katika Kijiji
cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja kipindi kilichopita.
Wataalamu na Mabingwa hao wa Sekta ya Afya kutoka
Baps Charities wanafanya uchunguzi wa maradhi mbali mbali pamoja na kutoa
dawa bure ikiwemo miwani za kusomea kwa Wananchi wanaofika kwenye Kambi hiyo.
Zaidi ya Wananchi 1,000 kutoka sehemu mbali mbali
za Majimbo na Shehia zilizomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” wamejitokeza
kufanya uchunguzi wa afya zao na kupatia dawa pamoja na ushauri.
|
Daktari dhamana ambae pia ni Mkuu wa Kitengo cha Macho Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Slim Mo’h Mgeni wa kwanza kutoka Kulia akimpatia maelezo Balozi Seif anayeshuhudia uchunguzi wa Macho katika Kambi ya afya iliyowekwa Kituo cha Afya Mahonda.
Balozi Seif akimvisha Miwani Mmoja wa Wananchi baada ya kumaliza kufanyiwa uchunguzi wa Afya na kubainika anahitaji kuwa na miwani ya kusomea.
Msongamano mkubwa wa Wananchi waliojitokeza kufanya uchunguzi wa Afya katika Kituo cha Afya Mahonda chini ya Madaktari na wataalamu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Baps Charities. Picha na OMPR – ZNZ.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...