Zaidi ya viwanda 400 vinatarajia kushiriki maonesho ya aina yake ya viwanda vya Tanzania, maonesho yenye lengo la kuitangaza na kuikuza sekta ya viwanda ili iweze kuchangia pakubwa katika uchumi wa taifa.

Maonesho hayo yanatarajia kuanza (kesho) Jumatano Desemba 07 na kufikia kilele chake Desemba 11 katika Uwanja wa maonesho ya Biashara ya kimataifa wa Mwl.J.K Nyerere maarufu kama Sabasaba jijini Dar es salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA),,Bwana Frank Kanyusi alisema jana jijini Dar es salaam kuwa, lengo la maonesho hayo ni kutekeleza azma ya serikali ya ya awamu ya tano, ya kuifanya Tanzania kufikia hatua ya kuwa nchi ya viwanda.

Bwana Kanyusi alisema maonesho hayo yatatoa fursa kwa viwanda vidogo, vya kati pamoja na viwanda vikubwa, kuonyesha bidhaa wanazozalisha nchini, na kutoa hamasa kwa watanzania kutumia bidhaa hizo.

“Tunataka wazalishaji kwenye viwanda vya chini hadi viwanda vikubwa, waje wawaonyeshe watanzania kile ambacho kinazalishwa, huku tukitarajia wananchi watahamasika katika kununua bidhaa hizi zinazozalishwa Tanzania,” alizema Bwana Kanyusi .

Alisema kusanyiko hilo la wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi, itakuwa fursa nzuri ya kutoa huduma mbalimbali zinazohusiana na uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara, huduma ambazo zitapatikana kwenye viwanja vya maonyesho na kutolewa na watendaji wa BRELA.

“Maonesho hayo ni fursa pia kwa washiriki na wananchi kupata huduma za haraka na za papo kwa papo zinazoihusu sekta za viwanda na biashara, kama vile usajili wa makampuni, alama na majina ya biashara, utoaji wa leseni za viwanda, pamoja na urasimishaji wa biashara, ” aliongeza.

Alisema BRELA itakuwa na banda maalum ambalo litatoa huduma hizo kwenye viwanja hivyo vya maonesho, na kuwataka washiriki na wananchi wengine wenye kuhitaji huduma za usajili ama leseni za viwanda vidogo na vikubwa, kutumia fursa ya maonesho hayo kupata huduma nyingi na za haraka zitakazotolewa muda wote wa maonesho hayo.

Akizungumzia urasimishaji wa biashara, Bwana Kanyasi alisema ni wakati muafaka kwa watanzania kufanya urasimishaji wa biashara zao, kwa lengo la kuwafanya waendeshe ama kumiliki biashara halali na inayotambulika kisheria, na hivyo kuwaondolea usumbufu usiokuwa wa lazima kutoka kwenye taasisi na vyombo mbalimbali vya serikali.

“Ni jambo la msingi kwa wafanyabiashara ama wamiliki wa viwanda na wazalishaji, kuzifanya biashara zao ziwe rasmi na kuhakikisha wanazisajili majina ama alama wanazotumia,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo itarahisisha bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania kupenya kirahisi sokoni ndani na hata nje ya nchi.

Maonyesho hayo yameandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali likiwamo Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Shirika la viwanda vidogovodogo (SIDO), Shirika la viwango Tanzania (TBS), pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Washirika wengine katika kuyaandaa maonesho hayo ni pamoja na Shirika la Maendeleo Tanzania (NDC), Ukanda huru wa uwekezaji (EPZA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Kampuni inayojihusisha na alama za biashara ya GSI, pamoja na wadau wengine toka Kisiwani Zanzibar, huku lengo likiwa ni kuharakisha ukuaji wa sekta ya viwanda na biashara nchini Tanzania.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Bw.Frank Kanyusi akizungumza jambo juu ya maonesho ya viwanda vya Tanzania yatakayoanza Desemba (kesho) 07 hadi Desemba 11 katika uwanja wa maonesho ya Biashara ya kimataifa wa Mwl.J.K Nyerere maarufu kama Sabasaba jijini Dar es salaam yenye lengo la kuitangaza na kuikuza sekta ya viwanda ili iweze kuchangia pakubwa katika uchumi wa nchi. BRELA itatoa huduma zake za urasimishaji wa biashara katika maonesho hayo.                

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...