Na Mwene Said wa Blogu
ya Jamii, Dar es Salaam.
Mwanzilishi-mwenza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media, Maxence Melo
Mubyazi (40), leo amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya
dhamana katika kesi moja kati ya tatu zinazomkabili ikiwamo ya kuzuia Jeshi la
Polisi kufanya uchunguzi na kuendesha mtandao wa Jamii Forum bila usajili.
Mapema jana asubuhi mshtakiwa huyo ambaye pia ni
mfanyabiashara na bosi wa mtandao huo, alifikishwa katika viunga vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mapema asubuhi.
Alipandishwa kizimbani saa 3:29 kusomewa mashtaka katika kesi yake
ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Mohamed Salum akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Yohanes
Kalungula.
Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi
na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa
akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media Ltd, inayoendesha mtandao wa kijamii
wa Jamiiforums, akiwa anajua polisi wanafanya uchunguzi kutokana na taarifa
zilizochapishwa katika mtandao huo, alishindwa kutoa taarifa. Ilidaiwa kuwa
mshtakiwa alishindwa kutoa taarifa ambazo ziko chini yake huku akijua ni kosa.
Mshtakiwa alikana shtaka hilo, upande wa Jamhuri ulidaia kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na haukuwa na pingamizi la dhamana hivyo
uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Simba alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na
wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika au serikalini, watakaotia
saini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 10 kila mmoja.
Mshtakiwa alitimiza masharti hayo dhidi ya kesi hiyo na imepangwa
kutajwa Desemba 29, mwaka huu.
Katika kesi ya pili, mshtakiwa alisomewa mashtaka yake
mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa. Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe
tofauti kati ya Mei 10 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar
es Salaam, mshtakiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamii Media Ltd,
inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums, huku akijua kwamba polisi
wanafanya uchunguzi kuhusu taarifa zilizochapishwa katika mtandao wake,
alishindwa kutoa taarifa hizo ambazo ziko chini yake. Mshakiwa alikana shtaka
hilo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
unaendelea na haukuwa na pingamizi la dhamana na uliomba tarehe ya kutajwa. Hata
hivyo, mshtakiwa katika kesi hii alishindwa kutimiza masharti ya dhamana kwa
kutokuwa na wadhamini na alirudishwa mahabusu hadi Desemba 29, mwaka huu kesi yake
itakapotajwa.
Katika kesi ya tatu, mkurugenzi huyo alipandishwa
kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Wakili Salum alidai kuwa katika tarehe tofauti, kati ya Desemba,
mwaka 2011 na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam,
mshtakiwa akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, aliendesha mtandao wa kijamii
ujulikanao kama Jamiiforums.com bila kuwa na usajili wa kuendesha mtandao huo.
Katika shtaka la pili, katika tarehe tofauti, kati ya Januari 26
na Desemba 13, mwaka huu eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa
akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo inayoendesha mtandao wa kijamii wa Jamiiforums
huku akijua kwamba polisi wanafanya uchunguzi kuhusu taarifa zilizochapishwa
katika mtandao wake alishindwa kutoa taarifa hizo ambazo ziko chini yake.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na
mashahidi wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana
ya Sh. Milioni Moja kila mmja pamoja na mshtakiwa. Mshtakiwa alitimiza masharti
hayo na kesi yake itatajwa Januari 16, mwaka 2017.

Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa JamiiForums, Maxence Melo akiongozwa na Askari Polisi wakati alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam leo, kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...