Mpiga picha maarufu Mpoki Bukuku amefariki dunia leo katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali akiwa akitokea kazini jana usiku maeneo ya Mwenge jijini Dar es salaam.

Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma (MOI) Almas Jumaa.

"Ni kweli Mpoki amefariki dunia mchana huu, alipokelewa jana usiku baada ya kupata ajali ya gari maeneo ya Mwenge  ITV, taarifa zaidi tutazitoa baadaye," alisema Almas.

Mpoki Bukuku amewahi kufanya kazi kama Mpiga Picha Mkuu katika gazeti la Mwananchi, linalochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Pia amewahi kufanya kazi magazeti kadhaa likiwemo Majira na Nipashe.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU 
MAHALI PEME PEPONI-AMIN

Tumepoteza nguzo 
katika tasnia ya habari

 Leo, kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusiana na kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Bw. Mpoki Bukuku (44), aliyefariki asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es salaam.
Kwa familia yake, wamempoteza baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari.


  Bukuku alikuwa ni mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa ni mtu aliyeipenda fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine wote ilimuweka matatani.


Wale wanaoelewa uandishi wa habari wa picha watabaini kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili za kila mpigapicha ili kupata habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na sifa zote hizo mbili. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake hasa wakati akifuatilia habari kubwa kokote kule katika nchi hii.


 Alipigwa na hata kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini bado mahaba yake katika kufanikisha habari bora hayakuzimwa. Alikuwa ni mwandishi wa habari siyo kwa bahati mbaya, bali ni kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza wajibu wake wa kutekeleza kazi mbalimbali za kihabari alizopangiwa na wahariri wake.


Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiuweledi, mara zote atakuwa nasi daima.


Sisi katika Kampuni ya The Guardian Limited tunaungana na famila, ndugu na marafiki katika kippindi hiki kigumu, kuombeleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi. Kampuni itaiunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku.


Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa The Guardian Limited, kwa heshima kubwa natoa salamu zangu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini Tanzania, kwa kifo cha ghafla na kushtua cha mmoja wetu.

Richard Mgamba
Mkurugenzi Mtendaji,
The Guardian Limited
Desemba 23, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...