Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la
kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika Jiji la
Mwanza mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha maandalizi ya maeneo
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia
Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es
Salaam huku akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo
hilo aachie ngazi.
"Kumeibuka tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa
Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi
wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata
kwa kufanya biashara, hili jambo sio sawa hata kidogo.
"Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye
hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa
biashara ndogondogo au Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza
kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja ya Watanzania, kwamba kuna
Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na
Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji, huo sio mwelekeo
wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe
(Makamu wa Rais) tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu
wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili
nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho" amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga walioondolewa
katika maeneo yao Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo
Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.
"Narudia na hii ni mara ya mwisho. Kawaambieni
hata Wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea
utaratibu mzuri. Kigamboni hapa palikuwa na Wamachinga eneo fulani wamehama
vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi
wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga, lakini
Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi
sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa" amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa
Iyombe.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini
kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha
Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na badala yake
wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji
anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.
"Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale,
kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili,
mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale
wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu."Na hizi
ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda
kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii akilini" amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa
kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo
kwa kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya
wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.
Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana
maana kuwa Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja
sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwakaribisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo aliyeambatana na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe kabla ya kuanza kwa kikao chao cha pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika kikao cha pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu mara baada ya kutoka kwenye kikao cha pamoja kilicho wahusisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kumaliza kikao chao kilicho wahusisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU
LAKINI MHESHIMIWA WATU WATAPITA KWENYE NJIA GANI??????? AU WENYE BIASHARA HALALI WATALIPA KWELI KODI?? HUU NI MKANGANYIKO SASA INA MAANA MTU UNAWEZA KUWEKA AU KUFUNGUA BIASHARA POPOTE HATA BARABARANI WATU WATAPITA WAPI??
ReplyDeleteDr. JPM wewe ni msomi hivo naamini unaamini utafiti pale ufunuo usipokuwepo. Toa fedha watafiti wa uchumi wagundue ni mahala papi wakiwekwa machinga watakaa na pia watapata wateja wengi zaidi. Hapo. Lakini si kuwajengea tu wakati sehemu hiyo haina wateja wataondoka na kuliacha jengo hilo.
ReplyDeleteMKUU WA NCHI IWAPO TUNAHITAJI MAENDELEO YA KWELI BASI HAPANA BUDI WATU WETU WASHIRIKISHWE,
ReplyDeleteDUNGU WAKUU WA MIKOA NA WILAYA, UTAFANIKIWA VINGI KATIKA DUNIA HII KUPITIA MATENDO YA REHEMA KULIKO KWA MATENDO YA KUADHIBU WATU.
DR. JAMESY
Nchi ya ajabu hii,sheria hakuna sasa hii inatufanya katika nchi zote za afrika mashariki sisi Tanzania ndiyo hatufuati sheria huwezi kufungua au kuweka biashara hata barabarani hii haikubaliki.tunakuwa nchi ya vurugu sasa huwezi kulinganisha miji mingine ya afrika na Dar es salaam wetu ni mchafu,hauna sheria,wapi Nairobi au Kampala mtu anaruhusiwa kujiwekea biashara popote ambako haparuhusiwi hii ni hatari.lazima tufuate sheria si kutafuta umaarufu wa kupata kura 2020.
ReplyDeleteMKUU WA NCHI NAONA UNAWABAGUA WAFANYABIASHARA UMEONA AU UMESIKIA KWENYE VYOMBO VYA HABARI WAZIRI WAKO WA MALIASILI NA UTALII ALIVYOBORONGA KUWAFUNGIA WAFANYABIASHARA WA VIUMBE HAI WAKATI WANALESENI NA WAMELIPIA VIBALI PAMOJA KUWA NA VIUMBE KWA HOLDING GROUND ZAO BILA KUWAJALI KUWA WATAPELEKA WAPI HAWA VIUMBE,AMEWAINGIZA KWENYE UMASIKINI NA KUWADHULUMU HAKI ZAO.WAPO WALIOKUWA NA MIKOPO SASA WANAUZIWA MALI ZAO NA MABENKI.HILI NI JAMBO LA KUSIKITISHA SANA TENA SANA,HATAKI KUWASILIZA HAWA WAFANYABIASHARA AMEJIAMULIA YEYE KAMA YEYE BILA KUFUATA HATA KUWASIKILIZA WATAALAMU WA WIZARA,NAFIKIRI KUWA ANAKUFANYA MKUU WA NCHI SERIKALI YAKO IONEKANA MBAYA KWA WAFANYABIASHARA
ReplyDelete