JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600 |
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Baadhi ya Vyombo vya
habari vya hapa nchini hivi karibuni vilitoa taarifa kuwa, Watanzania 8
wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa Serikali ya Tanzania wamekamatwa nchini Malawi
kwa tuhuma za kuingia kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera uliopo nchini Malawi
kinyume cha sheria.
Taarifa hiyo kwa mara ya
kwanza ilitolewa na chombo cha habari cha Malawi ambacho kilidai kuwa watu hao
wametumwa na Serikali ya Tanzania ili kuchunguza kama Serikali ya Malawi inatengeneza
silaha za nyuklia kwa kutumia madini ya urani ya kutoka mgodi huo.
Kufuatia taarifa hizo, Wizara
kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi ulifuatilia ili kubaini ukweli wa
tukio hilo. Baada ya kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka
taasisi ya CARTAS iliyo chini ya Kanisa Katoliki Songea mkoani Ruvuma walikamatwa
na vyombo vya usalama katika Wilaya ya Karonga ambayo inapakana na Wilaya ya
Kyela. Watanzania hao mara moja
walifunguliwa kesi kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia eneo la
mgodi bila kibali (criminal trespass).
Ubalozi uliwasiliana na
Taasisi ya CARTAS kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao kufanya ziara nchini
Malawi. Ubalozi ulielezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo walitaka
kufahamu juu ya madhara yatokanayo na machimbo ya madini ya urani. Watanzania
hao kwa sasa wapo katika gereza kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena
tarehe 04 Januari 2017.
Ubalozi unaendelea kufanya
mawasiliano na Kanisa Katoliki Songea ili kupata maelezo zaidi kuhusu ziara ya
watu hao kwa madhumuni ya kuyawasilisha mamlaka husika ili watuhumiwa waweze
kutolewa.
Aidha, Wizara kupitia
Ubalozi umebaini kuwa CARTAS iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini Malawi
bila kupata kibali kutoka mamlaka husika na bila kutoa taarifa Ofisi ya Ubalozi
kuhusu ziara hiyo.
Aidha, kipindi cha kufanya
ziara hiyo nchini Malawi hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya
Malawi wanakuwa katika likizo ya mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03
Januari 2017. Hii inakwamisha juhudi za kuwafuatilia watu hao ikiwa ni pamoja
na kukwama kwa maombi ya kibali cha kuwatembelea watu hao tarehe 28 Desemba
2016.
Wizara inatoa wito kwa
mara nyingine kwa taasisi za dini, vyuo vya elimu na watu binafsi kuomba vibali
na kufuata sheria za nchi nyingine wanapofanya ziara za mafunzo au ziara nyinginezo
ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya kufahamishwa
taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka
usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wizara, kupitia Ubalozi wa
Tanzania nchini Malawi unaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa suala hilo
linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
29 Desemba 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...