Na:
Lilian Lundo – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda
Yoweri Museveni kwa pamoja wamekubaliana kutosaini mkataba wa mahusiano ya
kiuchumi na kibiashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ulaya
(EPA).
Makubaliano hayo
yamefanyika jana Ikulu, Jijini Dar es Salaam ambapo Rais Yoweri Museveni yuko nchini Tanzania kwa
ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 25 – 26 Februari, 2017.
Akiongea na waandishi
wa habari Rais Magufuli amesema kuwa mkataba wa EPA hauna faida bali ni aina
nyingine ya ukoloni ambao unataka kurejeshwa kwa nchi za Afrika.
“Nimeongea na Rais
Yoweri Museveni amekubali kutosaini mkataba wa EPA, nitawaagiza wataalamu
waliosaidia kutupa maelezo juu ya madhara ya mkataba huo kwenda pia Uganda
kuwapa maelezo ambao waliyatoa kwa Tanzania,” alifafanua Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake, Rais
Yoweri Museveni amesema kuwa ameongea na Rais Magufuli na wamekubaliana kutosaini
mkataba huo na kuongeza kuwa suala la EPA ni lazima lijadiliwe na nchi zote za Afrika
Mashariki ili kuwepo na msimamo wa pamoja kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Aidha Rais Museni amempongeza
Rais Magufuli kwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege
mpya Sita, hivyo amekaribisha shirika hilo kutoa huduma za usafiri wa anga
nchini Uganda kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji wa huduma hiyo.
Vilevile amempongeza
Rais Magufuli kwa ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge
Railway) kutoka Dar es Salaa mpaka Mwanza na Isaka mpaka Rwanda ambapo
itapelekea ujenzi wa bandari kavu katika mkoa wa Mwanza hivyo wafanyabiashara
wa Uganda kunufaika na bandari hiyo ambayo itakuwa karibu zaidi kuliko ilivyo
kwa Dar es Salaam.
Wakati huohuo
Mawaziri wa Nje kutoka Tanzania na Uganda Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Oryem
Henry Okello wamesaini makubaliano ya uhusiano katika mambo ya Diplomasia baina
ya nchi hizo mbili.
Museveni yupo nchini
kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo atatembelea baadhi ya maeneo kadhaa
ikiwemo kiwanda cha Juice cha mfanyabiashara Mtanzania Said Bakhressa ambaye pia
amewekeza nchini Uganda.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni
alipowasili Ikulu jijini Dar es salaam kuanza ziara rasmi ya kiserikali
ya siku mbili leo Februari 25, 2017 .
PICHA NA IKULU
PICHA NA IKULU
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...