Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Machi 8 Mwaka huu, katika uwanja wa Mwembeyanga Temeke Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jana maadhimisho hayo yataongozwa na maandamano ya Wanawake na wadau mbalimbali, na yataanzia katika Shule ya Msingi Mabatini kuelekea viwanja vya Mwembeyanga.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania ya viwanda, Wanawake ndio Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi”.

Kauli mbiu hiyo inalenga kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi kwa Wanawake hasa kutambua mchango wao katika kuleta Maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.

Taarifa hiyo pia imeikumbusha jamii kuhusu wajibu wake ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha, kuwaamini na kuwapa Wanawake haki sawa katika nafasi za Elimu, Uchumi na uongozi ili wawe chachu ya mabadiliko yenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya kazi za ujasiriamali yanayoendelea katika uwanja wa Mwembeyanga, ambapo Asasi za kiraia na vikundi mbalimbali vya wanawake vitaonesha bidhaa zao.

Aidha, Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam wanakumbushwa kushiriki kwa wingi katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kuwa na mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinanazowakabili Wanawake kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...