Tanzania imeshiriki
katika Mkutano ulioitishwa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
inayoshughulikia masuala ya Nchi Masikini Duniani kushiriki katika Mkutano wa
kujadili utekelezaji wa Programu ya Istanbul (Istanbul Programme of Action - IPOA)
kwa nchi zilizo kwenye kundi la nchi masikini barani Afrika.
Mkutano huo umefanyika
kwenye Hoteli ya Radisson Blu, Dakar, Senegal kuanzia tarehe 28 Februari hadi 1
Machi 2017.
Ujumbe wa Tanzania katika
Mkutano huo umeongozwa na Mhe. Bi. Maria
Leticia Sasabo, Katibu
Mkuu (Sekta ya Mawasiliano), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Wajumbe
wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Bw. Jestas A. Nyamanga, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya
Ushirikiano wa Kimataifa , Injinia Nikusubila Maiko ; Mtaalamu wa Masula ya Mkongo Mawasiliano na Bw. Abilah Hassan Namwambe, Afisa Mambo ya Nchi za Nje, anayeshughulikia masuala ya
Kundi la Nchi Masikini Duniani kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki.`
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Kufanikisha utekelezaji wa Programu
ya Istanbul ndani ya mustakabali wa Ajenda 2030 ya Maendeleo Endelevu”
(Accelerating the implementation of the Istanbul Programme of Action within the
Context of the 2030 Agenda: A focus on broadband connectivity).
IPOA ilizinduliwa na Jumuiya ya Umoja wa Mataifa mwaka 2011 kwa lengo la kumaliza tatizo la umasikini
kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka
2020.
Hadi sasa, Mpango huo
unakaribia kuisha muda wake lakini tatizo la umasikini bado ni kubwa na pia
idadi ya nchi zilizo kwenye kundi la nchi masikini duniani imeongezeka badala
ya kupungua.
Katika Mkutano huo, Wajumbe
kutoka nchi mbalimbali Duniani, wamejadili masuala ya matumizi ya Mkongo wa
Mawasiliano ya Mtandao “BroadBand Connectivity”, kama nyenzo muhimu ya kuleta
maendeleo.
Mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa Mataifa mbalimbali na wadau wa
maendeleo wamejadili na kuweka mikakati mipya ya namna bora ya kufanikisha na kuharakisha utekelezaji wa
malengo yaliyoazimiwa kwenye IPOA. Aidha, Mkutano huo umeainisha matokeo ya utafiti
uliofanywa kuhusu matumizi ya Mkongo wa Mawasiliano katika nchi za Rwanda na
Senegal.
Vilevile, matokeo ya
Mkutano huo yatazingatiwa kama maoni katika Jukwaa la Ngazi ya Juu la Kisiasa, High Level Political Forum litakaloitishwa na Baraza
la Umoja wa Mataifa la Uchumi na Jamii (Economic and Social Council)
litakapofanya mapitio
ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo Julai, 2017.
Tanzania imetajwa kuwa
miongoni mwa nchi chache zilizopiga hatua kubwa sana katika kuwaletea wananchi
wake Maendeleo hasa katika sekta ya Mawasiliano.
Ujenzi wa Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano, Huduma za kifedha, na za kibenki kwa kutumia mitandao na simu
za mkononi na gharama ndogo za huduma za simu na kimtandao ni baadhi tu ya
maeneo ambayo Tanzania inaongoza kwa kufanya vizuri.
Wa tatu
kutoka kushoto ni Mhe. Mama Maria Leticia
Sasabo, Katibu Mkuu (Sekta ya Mawasiliano), Wizara akifuatiwa na Bw. Jestas A. Nyamanga Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mmabo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wajumbe kutoka nchi nyingine wakifuatilia mada
mbalimbali katika Mkutano huo.
Bw. Abilah Hassan Namwambe, Afisa Mambo ya Nchi za Nje, anayeshughulikia masuala
ya Kundi la Nchi Masikini Duniani kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, akiwa katika maandalizi ya Mkutano huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...