Na Veronica Simba - Dodoma
Serikali imeitaka Kampuni ya PR NG Minerals Limited ya Australia,
inayofanya utafiti wa madini adimu (rare earth elements), eneo la
Ngualla mkoani Songwe, kukamilisha utafiti huo haraka ili waanze
uzalishaji mapema iwezekanavyo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alimwambia
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Dave Hammond, aliyemtembelea ofisini
kwake mjini Dodoma jana kuwa, Serikali imedhamiria kuachana na
utamaduni au mazoea ya kujikita kwenye uzalishaji wa madini ya
kawaida pekee badala yake inataka kuanza uzalishaji wa madini adimu
pia ili kuendana na Soko la Dunia.
“Hivi sasa Dunia nzima inageukia kwenye uzalishaji wa madini adimu,
hivyo nasi ni lazima tuanze uzalishaji wake mapema iwezekanavyo.”
Aidha, Waziri Muhongo aliitaka Kampuni hiyo kuwasilisha Mpango Kazi
wake ambao pamoja na mambo mengine utaonesha ni lini uzalishaji
utaanza.
Akifafanua umuhimu wa kubainisha Mpango Kazi wa Kampuni hiyo,
Profesa Muhongo alibainisha kuwa, baadhi ya wawekezaji katika sekta
ya madini hapa nchini, wamekuwa wakishikilia leseni za madini kwa
muda mrefu pasipo kuzifanyia kazi hivyo kuilazimu Serikali
kuwanyang’anya kwa mujibu wa Sheria ya Madini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo aliyeambatana na Meneja wa
Masoko wa Kampuni husika, Ismail Diwani, alimhakikishia Waziri
Muhongo kuwa watakamilisha utafiti wao na kuanza uzalishaji mapema
iwezekanavyo.
Mkurugenzi Hammond aliongeza kuwa, kupitia Mradi huo wa madini
adimu wa Ngualla, upo uwezekano wa Tanzania kuwa msambazaji
mkubwa wa kimataifa wa madini hayo.
Madini adimu yanajumuisha kundi la metali muhimu 17 ambazo ni
pamoja na Neodymium, Praseodymium, Scandium na Thulium.
Mojawapo ya matumizi yake ni katika magari yanayotumia umeme
pamoja na kutengenezea vifaa vya kisasa vya kielektroniki.
Kwa Tanzania, madini adimu yanapatikana katika mikoa ya Songwe,
Mbeya na Morogoro.
Mkurugenzi wa Kampuni ya PR NG Minerals Limited, Dave Hammond
(wa pili kutoka kushoto), akifafanua jambo kwa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) wakati wa mazungumzo
yao yaliyofanyika jana ofisini kwake – Makao Makuu ya Wizara mjini
Dodoma. Wengine kutoka kulia ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi
Rayson Nkya, Mjiolojia Mkuu kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST),
Alphonce Bushi na Meneja wa Masoko wa Kampuni husika, Ismail
Diwani.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto),
akisisitiza jambo kwa Ujumbe kutoka Kampuni ya PR NG Minerals,
waliomtembelea ofisini kwake jana – Makao Makuu ya Wizara, mjini
Dodoma.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...