Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 31 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Ziara ya Mhe. Dessalegn inakuja kufuatia mkutano kati yake na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu.

Mhe. Dessalegn anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 31 Machi, 2017 asubuhi na atapokelewa na Mhe. Rais Magufuli. 

Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Jioni ya siku hiyo, Mhe. Dessalegn na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.

Tarehe 01 Aprili, 2017 Mhe. Dessalegn ataendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
30 Machi, 2017
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (katikati), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya ziara ya siku mbili ya kitaifa ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini. Waziri Mkuu huyo atawasili nchini tarehe kesho 31 Machi, 2017 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Akiwa nchini atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kutembelea Bandarini. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Balozi Naimi Aziz (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Innocent Shiyo (kulia). 
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Aziz naye akielezea jambo wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...