Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 25 Oktoba, 2017 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi watatu
waliopangiwa kuziwakilisha nchi za Oman, Uholanzi na China hapa nchini.
Waliowasilisha hati zao kwa Mhe. Rais Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam ni
Mhe. Ali Abdullah Al Mahruqi – Balozi wa Oman hapa nchini, Mhe. Jeroen Verheul
– Balozi wa Uholanzi hapa nchini na Mhe. Wang Ke – Balozi wa China hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi
zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itafanya kazi nao kwa
ukaribu ili kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo na Tanzania
hususani katika uchumi.
“Nimefurahishwa sana na ziara iliyofanywa na Mawaziri wa Oman hapa nchini,
naomba ufikishe shukrani zangu kwa Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin
Said Al Said, naamini yote tuliyozungumza ikiwemo kubadilishana uzoefu katika
mafuta na gesi, uwekezaji katika viwanda na ujenzi wa miundombinu tutayatekeleza
kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu” amesema Mhe. Rais Magufuli
alipozungumza na Balozi Ali Abdullah Al Mahruqi wa Oman.
Mhe. Rais Magufuli amemuambia Balozi Jeroen Verheul wa Uholanzi kuwa
Tanzania inayo gesi nyingi na itafurahi kupokea wawekezaji kutoka Uholanzi
ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ina uzoefu na teknolojia kubwa katika sekta hiyo.
Kwa upande wa Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Mhe. Rais Magufuli
amesema uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na kidugu, hivyo ametoa
wito kwa Balozi huyo kuuendeleza na kuhakikisha fursa zenye manufaa kwa nchi zote
zinatumiwa ipasavyo ikiwemo kukuza uwekezaji, biashara, utalii na ushirikiano katika
usafiri wa anga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
25 Oktoba, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Ikulu jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkuu wa Itifaki Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Grace Alfred Martin
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akitazama vitabu alivyokabidhiwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa Uholanzi hapa nchini Mhe. Jeroen Verheul Ikulu jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Itifaki Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Grace Alfred Martin
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Oman hapa nchini Mhe. Ali Al Mahruqi Ikulu jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkuu wa Itifaki Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Grace Alfred Martin
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...