Na Tulizo Kilaga, Kilwa

MKUU wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Christopher Ngubiagai amewataka wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi kushirikiana kwa ukaribu na kwa uharaka na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kutatua migogoro ya mipaka ya misitu ili kuepusha migogoro.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya huyo alipokua akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo anayefanya ziara yake katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Ngubiagai amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ina tatizo kubwa la suala la mipaka ya misitu kati ya kijiji na kijiji, TFS na kijiji na hasa baada ya vijiji kunufaika na mapato yatokanayo na uhifadhi wa misitu ya hifadhi, vijiji n.k.

“Mara ya mwisho nilikwenda kijiji cha Mchakama ambapo ramani zinaonyesha kabisa wananchi watakiwa wawepo katika eneo hili lakini wananchi wanasema hapana sisi mpaka tunaoutambua ni huu hivyo tunaomba Wizara ya Ardhi watusaidie kutatua tatizo ili tuweze kuendelea mbele zaidi,” alisema Ngubiagai.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TFS Prof. Dos Santos Silayo alisema wakati mwingine migogoro inatokea kutokana na kutokushirikishana na hasa kwa NGOs zinapokwenda kusaidia miradi katika vijiji bila kujali kuwa kuna mamlaka nyingine zenye mashiko na ardhi husika na hivyo kusababisha misuguano.

Prof. Silayo aliomba Wakuu wa Wilaya nchini kuwabana wale wote wanaoanzisha miradi kwenye maeno yao pasipo kuwa na ushirikishwaji wa kutosha wa wataalamu wao na hivyo kuigombanisha serikali na wananchi wake pindi wananchi wanapotakiwa kuondoka kwenye maeneo waliyovamia na hasa katika maeneo ya misitu.

Mkazi wa Kilwa Masoko, Ramadhani Hamisi alisema migogoro mingi ya ardhi katika maeneo ya misitu inatokana na sekta ya misitu hapo nyuma kushindwa kutekeleza majukumu yake hali iliyopelekea maeneo mengi ya msitu kugeuzwa shamba la bibi hadi pale ilipoanzishwa TFS na kujengewa uwezo wa kusimamia misitu hali iliyorudisha hadhi ya misitu mingi nchini.

Desemba 2015 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanaongeza udhibiti na usimamizi wa migogoro ya ardhi kwenye maeneo yao husika.
MKUU wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Christopher Ngubiagai (dulia) akimwelezea Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo changamoto mbalimbali za uhifadhi wa misitu iliyopo Kilwa mapema wiki hii, Mtendaji kuu yuko kweneye ziara yake katika kikazi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...