Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
Bw.Richard Mayongela (wa tatu kulia), jana akiandika mambo mbalimbali katika mkutano na
wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza. Wa pili kushoto ni Meneja wa kiwanja hicho Bi.
Esther Madale na wa kwanza kulia ni Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Agustino
Magele.
Bw. Edger Mwankuga aliyesimama jana akiwasilisha hoja zake mbalimbali mbele
ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard
Mayongela (hayupo pichani) alipokutana na wafanyakazi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza na
Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.
Wafanyakazi wa idara mbalimbali za kiwanja cha ndege cha Mwanza na kikosi cha
zimamoto na uokoaji, wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela alipokutana nao jana kujadili masuala mbalimbali ya
kiuendeshaji.
Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wataendelezwa kwa kupata mafunzo
mbalimbali, ili kuongeza weledi na tija kazini, imeelezwa.
Kauli hiyo ambayo ni moja ya malengo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard
Mayongela jana alipoongea na wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza pamoja na Kituo cha
Zimamoto na Uokoaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.
Bw. Mayongela alisema wafanyakazi wakipata mafunzo zaidi ya kazi zao wataisaidia serikari kufanikisha
moja ya malengo yake makuu ya kukuza uchumi, ambapo watakuwa na mbinu za kisasa zikiwemo za
ukusanyaji wa mapato kwa uaminifu na uadilifu, ambapo viwanja vya ndege ni moja ya vyanzo vya
mapato hayo.
Hata hivyo, alisema atapitia majalada ya wafanyakazi wote ili kubaini waliojiendeleza kwa mafunzo
mbalimbali, lakini wanafanyakazi zisizo za kada zao, hivyo ataangalia uwezekano wa kuhamishiwa
kwenye kada zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi zaidi.
“Wapo wafanyakazi wa kada mbalimbali waliojiendeleza, lakini hadi sasa bado wapo kwenye kada
walizoajiriwa nazo na zipo tofauti na sasa, nitangalia uwezekano wa kupangiwa kada zao ili waweze
kuenda na kasi ya kazi zinazowahusu,” alisema Bw.Mayongela.
Pia malengo yake mengine alisema atahakikisha anaboresha maslahi ya wafanyakazi wa ngazi ya chini ili
kunyanyua ari na tija kazini, ambapo kwa sasa wamekata tamaa kutokana na maslahi duni yasiyolingana
na kazi zao.
Lakini aliwaasa wafanyakazi wenye mamlaka ya kuingia mikataba na wafanyabiashara, kubadilika na
kuhakikisha wanatumia vyema sheria zinazowaruhusu kuingia mkataba baina yao na sio kukiuka, kwani
inaweza kuwaletea matatizo, endapo itabainika kuwepo kwa udanganyifu uliosababisha upotevu wa
mapato ya serikali, kwa kuwa atahakikisha TAA inajitosheleza kimapato na kujiendesha kwa baadhi ya
mambo ya ndani bila kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.
Alisema kwa sasa TAA imekuwa ikinyooshewa kidole kwa kusemwa vibaya na wadau mbalimbali, lakini
kupitia umoja na mshikamano wa wafanyakazi atahakikisha anarudisha taswira nzuri iliyokuwepo na
kujenga Mamlaka mpya yenye kuaminika.
Pia alizungumzia uadilifu na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi, kuacha mara moja vitendo
vinavyoweza kuhujumu jitihada na vipaumbele kwa mwaka huu wa fedha 2017/18 hadi kufikia 2020/21.
“Mimi ni mgeni katika nafasi hii (ya Ukurugenzi), lakini ninachoomba tufanye kazi kwa bidii, mvunje
makundi na tukosoane kwa kujenga na sio kubomoa, na viongozi muache kupendelea mtende haki kwa
wafanyakazi wote, tukiwa na lengo la kuijenga TAA yenye mwelekeo mpya,”alisema Bw. Mayongela.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...