Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Dkt. Hassan Abbas amewahamasisha Waandishi wa Habari wa
Tanzania kushiriki vema katika kuwania tuzo za wanahabari wa Jumuiya
za Mendeleo Kusini mwa Bara la Africa (SADC).
Dkt. Abbas ametoa rai kwa Waandishi wa Habari kushiriki tuzo hizo
jumatatu wiki hii wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu hali
ya uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo nchini.
“Tunawaomba wale wote ambao wanadhani wanavigezo basi washiriki
tuzo hizi za umahiri ambazo zinahusu waandishi wa habari za magazeti,
redio, televisheni na wapiga picha za habari”, alieleza Mkurugenzi wa
Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Alieleza kuwa maelezo kamili juu ya tuzo hizo yanapatikana katika
tovuti ya Idara ya Habari ya www.maelezo.go.tz hivyo wote wenye
habari mahiri katika magazeti, vipindi vizuri vya luninga au wapiga picha
wahakikishe wanashiriki ili kushindana na waandishi wenzao kutoka
nchi za kusini mwa Afrika.
Mbali na tuzo za SADC, Dkt. Abbas pia ameeleza kuwa tuzo nyingine ya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
inashindaniwa na Wanahabari na maelezo yake yanapatikana katika
tovuti ya Idara ya Habari.
Amewataka wanahabari kuandika habari zao kwa umahiri mkubwa
ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaweza kukidhi hata kupata
tuzo za waandishi bora kama hizo zilizojitokeza.
Pamoja na kuwataka waandishi wa habari kushiriki katika tuzo hizo, pia
amewataka waandihsi hao kuhakikisha wanapata vitambulisho vipya ya
Waandishi wa Habari (Press Cards) vya mwaka 2018 baada ya vile vya
mwaka jana kuisha muda wake.
“Kwa kweli mwaka huu tutakuwa wakali kidogo kwa wale ambao
hawatokuwa na vitambulisho hivi kwani mchakato wa kuvipata ni rahisi
kwa sababu tumeshawapa muda wa miaka mitano wa kwenda kusoma
hivyo hatuhitaji vyeti, kinachohitajika ni barua ya mwajiri au chombo
cha habari unachofanyia kazi tu.” Alisema Dkt. Abbas.
Aidha, Dkt. Abbas amewakumbusha wanahabari ambao bado kiwango
chao cha elimu kipo chini ya kile kilichowekwa katika Sheria ya Huduma
za Habari namba 12 ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017
kujiendeleza kwani muda uliotolewa wa miaka mitano unaendelea
unazidi kuisha.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...