Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

MFANYABIASHARA Boniface Mbilinyi (32) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka kutamka uongo wa kiasi cha fedha alichokuwa nacho.

Mbilinyi anadaiwa kutamka kuwa na dola za Kimarekani 40,000 huku akiwa na dola 123,000. 

Mwendesha mashtaka wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa amedai hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi kuwa Januari 13, mwaka huu,  katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Jk Nyerere uliopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar Es Salaami mshtakiwa alitenda kosa.

Amedai wakati mshtakiwa huyo akisafiri  kutoka nje ya Tanzania alitoa tamko la uongo kuhusiana na kiasi cha fedha alichokuwa nacho kwa kudai kuwa alitamka  kuwa ana kiasi cha dola 40,000 wakati ukweli alikuwa na dola 123,000.

Hata hivyo, mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika na wapo tayari kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali (PH).

Wakili wa mshtakiwa huyo, Ndigwako Joel alieleza mahakama kuwa hawajajiandaa kwa leo kusikiliza PH, hivyo aliomba wapewe tarehe ya karibu.

Pia aliiomba Mahakama impatie mteja wake kwa sababu shtaka linalomkabili linadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Wakili Mbagwa alidai wao kama upande wa mashtaka hawapingi dhamana ila aliikumbusha Mahakama wakati ikitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo izingatie kifungu cha 148(5)(e) kinachoelekeza mshtakiwa anayetuhumiwa na kiasi cha fedha kinachozidi Sh 10 milioni ni lazima alipe nusu ya kiasi hicho cha fedha.

Pia aliomba kiasi hicho cha fedha kilichopo katika hati ya mashtaka kisitumike kama sehemu ya dhamana kwa mshtakiwa huyo.

Baada ya kuwasilishwa kwa hoja hizo, Hakimu Shaidi alisema kwa kuwa fedha hizo zipo mikononi kwa Serikali, aliamuru mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua na kitambulisho na fedha hizo zitasimama kama bondi.

Kesi imeahirishwa hadi Februari 7, 2018.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...