Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Mstaafu, Projest Rwegasira
(wapili kushoto) akimsikiliza Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Askari Magereza,
Mhandisi Khadija Salum, alipokua anamuonyesha Katibu Mkuu huyo maeneo mbalimbali ya
ujenzi wa nyumba hizo zilizopo Ukonga, jijini Dar es Salaam. Katibu Mkuu huyo aliiagiza TBA
kumaliza ujenzi huo kwa muda wa miezi mitano kuanzia sasa.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Mstaafu,
Projest Rwegasira ameiagiza Wakala wa Majengo Nchini (TBA) ambao wanajenga
nyumba za askari wa Jeshi la Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam,
kuukamilisha mradi huo ndani ya miezi mitano kama walivyoahidi.
Katibu Mkuu huyo alitoa agizo hilo, jijini Dar es Salaam jana, wakati alipokua
akizungumza na Maafisa wa TBA pamoja na wa Jeshi la Magereza mara baada ya
kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo katika eneo zinapojengwa nyumba hizo,
akiwa na lengo la kujua ujenzi ulipofikia mpaka sasa.
“Licha ya maelezo yenu mlioyatoa jinsi mradi huu wa ujenzi unavyoendelea,
nimeyasikiliza vizuri, na pi nimeona hatua ya mradi huo ulipofikia, ila fanyeni juu
chini muhakikishe mradi huu unakamilika ndani ya miezi hiyo mitano mlioisema
hapa nyie wenyewe, muongeze nguvu zaidi katika kuukamilisha mradi huu kwa
wakati,” alisema Rwegasira.
Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 10 ambazo zilitolewa na Rais John
Magufuli mara baada ya kufanya ziara yake Ukonga mwishoni mwa mwaka juzi
na kutoa maelekezo wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari hao katika eneo
hilo.
Aidha, kutokana na agizo alilolitoa Katibu Mkuu huyo ambaye ndio msimamizi
mkuu na mwenye mradi huo na kukubaliana na TBA katika maelekezo hayo, hivyo
ifikapo mwezi Juni mwaka huu, mradi huo unatarajiwa kukamilika.
Ujenzi huo ulianza rasmi mwanzoni mwa mwaka jana 2017, mara baada ya
Desemba 19 mwaka juzi 2016, Mtendaji Mkuu wa TBA pamoja na Mkuu wa Jeshi
la Magereza nchini, walikutana na kusaini mkataba wa makubaliano wa kuanza
kwa ujenzi wa nyumba hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...