Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kuwa taarifa zinazosambaa mitandaoni
kuhusu sekta ya kibenki nchini kutokuwa salama si sahihi na zinapaswa kupuuzwa. Sekta ya
kibenki nchini ipo salama na Benki Kuu ipo makini kuhakikisha kuwa sekta ya kibenki na
mfumo wa fedha kwa ujumla ni salama na stahimilivu.
Benki Kuu inaendelea kuzisimamia
benki zote kwa ukaribu kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za
Fedha ya mwaka 2006. Taarifa zinazosambaa kuhusu kufungwa kwa benki zenye viwango
vikubwa vya mikopo chechefu (non-performing loans) hazina ukweli wowote. Taarifa hizo
zina lengo la kupotosha umma na kusababisha taharuki kwa wananchi. Benki Kuu
inawakumbusha wananchi kuwa benki ndiyo sehemu salama ya kuhifadhi fedha zao.
Benki Kuu inapenda kuuhakikishia umma kuwa haina lengo la kufuta leseni za benki bila
sababu za msingi kama inavyopotoshwa kwenye mitandao ya kijamii. Ni lengo la Benki Kuu
kuona kuwa benki zote zilizopewa leseni zinafanya vizuri. Aidha, ieleweke kuwa Benki Kuu
hufuta leseni ya benki pale tu benki husika inaposhindwa kuzingatia vigezo ambavyo
vimewekwa kisheria. Miongoni mwa sababu za msingi zinazoweza kusababisha kufutwa kwa
leseni ya benki ni kuwa na mtaji chini ya kiwango kinachotakiwa kisheria, upungufu wa ukwasi
na ukiukwaji wa sheria mbalimbali za kibenki, na si vinginevyo.
Benki Kuu itaendelea kusimamia shughuli za kibenki kwa ukaribu na kwa mujibu wa Sheria
ili kuhakikisha amana za wateja zinakuwa salama muda wote. Hivyo, wananchi wanaombwa
kuwa na utulivu na kuondokana na taharuki inayosababishwa na watu wachache. Pia Benki
Kuu inawakumbusha wananchi kutoziamini taarifa zisizo rasmi kuhusu usalama wa sekta ya
kibenki nchini Tanzania.
Taarifa rasmi kuhusu sekta ya kibenki hutolewa na Benki Kuu ya
Tanzania ambayo kisheria ndiyo msimamizi wa sekta hiyo nchini.
Wananchi wanakumbushwa kuwa usambazaji wa taarifa zisizo rasmi ni kinyume cha Sheria
ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na hatua kali zitachukuliwa kwa atakayebainika
kufanya hivyo.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
info@bot.go.tz
Januari 9, 2018
BENKI KUU YA TANZANIA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...