Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Willium Lukuvi
amesema Dar es Salaam ndio inaongoza kwa migogoro mingi ya ardhi
nchini.
Amesema ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi ameanzisha
kampeni inayofahamika kwa jina la Funguka na Waziri itakayotoa fursa
kwa wananchi wenye migogoro kuifikisha wizarani na hatimaye kupata
ufumbuzi.
Lukuvi amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na
waandishi wa habari kuhusu hatua ambazo Wizara yao inachukua
kutatua migogoro ya ardhi nchini.
Amesema Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi
imedhamiria kushughulikia migogoro ya ardhi nchini na kwa mwaka
huu yeye pamoja na Naiu Waziri wa wizara hiyo watazunguka maeneo
mbalimbali nchini kuwasikiliza wananchi na kutatua migogoro iliyopo.
Kuhusu Dar es Salaam ,Lukuvi amesema ni Jiji ambalo linaongoza kwa
migogoro ya ardhi nchini na kufafanua na wilaya inayoongoza ni
Kinondoni hasa maeneo ya Tegeta na Mbezi.
"Siku chache zilizopita nimeshughulikia migogoro ya ardhi kwa Mkoa
wa Dar es Salaam ambapo wananchi zaidi ya 400 nimewasikiliza na
kupata ufumbuzi.Na leo hii nimerudi tena Dar es Salaam ambapo kwa
leo tu wananchi 420 nitawasikiliza.
"Kwa Dar es Salaam migogoro inatokana na watu kudhulimiwa
viwanja, mirathi na mingine watu kuvamia viwanja vya watu wengine na
kisha kujenga.Pia ipo migogoro inayoshughulikiwa na Mahakama na
iliyotolewa hukumu.
"Migogoro ambayo imetolewa hukumu wizara haina uwezo wa
kuishughulikia ,hivyo tunashauri warudi tena mahakamani ili kupata
haki. Hivyo tutaendelea kuishughulikia kadri ya uwezo wetu.Tutafanya
hivyo kwa nchi nzima,"amesema Lukuvi.
Amefafanua leo, kesho na keshokutwa atakuwa Dar es Salaam na
baada ya hapo atakwenda Kagera na kisha atarudi tena Kanda ya
Pwani ambapo kuna Dar es Saalam na Pwani.
Akielezea zaidi jitihada zinazofanywa na wizara yake kutatua mgogoro
ya ardhi, Lukuvi amesema wakati yeye na Naibu Waziri wakiendelea
kushughulikia migogoro hiyo, pia watalaamu wa ngazi mbalimbali
wizarani hapo nao wanaishughulikia.
"Ipo migogoro ambayo Waziri wa Ardhi anao uwezo wa kuitafutia
ufumbuzi kutokana na mamlaka niliyonayo na ndio maana nimeamua
kuwa na kampeni ya Funguka na Waziri ili kusikiliza wananchi.Hivyo
kwenye kampeni kuna fomu maalumu ambazo zitajazwa na wananchi
na tukifika kwenye mkoa husika watajulishwa ili tuwasikilize.
"Na kwa kuwa tutakuwa tunasikiliza wananchi maeneo ya wazi ,hivyo
hata wale ambao watakuwa hawajaandikwa majina nao
watasikilizwa,"amesema.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...