MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Hudson Kamoga kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo wakati wanapowatumikia wananchi wa eneo hilo. 
RC Mnyeti akizungumza kwenye majumuisho ya ziara yake ya siku tano ya kutembelea halmashauri ya wilaya hiyo, alisema viongozi hao wanastahili pongezi kutokana na utendaji kazi bora wao kwa jamii. 
Alisema tangu akiwa mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kabla ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mkuu wa Mkoa wa Manyara, alikuwa anawasiliana na DC Mofuga kutokana na utendaji kazi bora anaoufanya. 
"Mheshimiwa mkuu wa wilaya kupitia nafasi hii nakupongeza kwa dhati kutokana na utendaji kazi wako, na nakutakia kila la heri ili siku moja upande cheo uwe mkuu wa mkoa," alisema Mnyeti. 
Alisema DC Mofuga ni kiongozi mwadilifu mwenye kuwatumikia wananchi wa Mbulu hivyo viongozi na wananchi wa wilaya hiyo wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha.
“Ukiona kiongozi anabishana na mkuu wa wilaya basi huyo atakuwa na matatizo, wewe mkuu wa wilaya chapa kazi kwani hakuna mtu mwenye mapembe au sharubu kwenye wilaya hii ya Mbulu zaidi yako wewe Mofuga,” alisema Mnyeti.
Alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga ni kiongozi mchapakazi anayetekeleza wajibu wake ipasavyo na miaka ijayo atapandishwa cheo na Rais John Magufuli.
“Mkurugenzi wewe chapa kazi, Rais ana vyombo vyake vingi vya uchunguzi atakuona tuu hata kama hayupo hapa kuna watu wake wanaandika andika na kufikisha taarifa ipo siku atakuona zaidi na kukupandisha cheo,” alisema Mnyeti.
Alisema Kamoga japokuwa ana muda mchache tangu ateuliwe na Rais Magufuli kushikilia nafasi hiyo ametimiza wajibu wake ipasavyo kwa kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao huku akisimamia vyema miradi ya maendeleo.
“Sina shaka na uadilifu wako kwani unafanya kazi kwa uadilifu umeanza vizuri wewe chapa kazi, mimi nilikuwa mkuu wa wilaya na leo ni mkuu wa mkoa kutokana na kufanya kazi hivyo fanya kazi utapanda cheo tuu,” alisema Mnyeti.
Alisema Kamoga ameanza kazi yake ya ukurugenzi wa halmashauri vizuri hivyo aendelee hivyo hivyo kwa kuwasimamia vyema wakuu wa idara ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa kuwatumikia.
Hata hivyo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza maelekezo na maagizo yote alioyatoa kwenye ziara hiyo kwa kadiri muda alioupanga ili kuhakikisha wananchi wanapata majawabu ya changamoto na matatizo waliotoa kwa kutimiziwa kwa wakati muafaka.
 Wakazi wa Kata ya Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, wakiwa wamepanda juu ya mti wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti akizungumza nao.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akiwa amembeba mtoto wa jamii ya Hadzabe wa bonde la Yaeda Chini, alipotembelea eneo hilo kwenye ziara yake ya siku tano, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Celestino Mofuga.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexanda Pastory Mnyeti akizungumza na wananchi wa bonde la Yaeda Chini kwenye ziara yake ya siku tano Wilayani Mbulu ya kuzungumza na wananchi, kukagua miradi na kuwasilikiza wananchi.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akizungumza kwenye bonde la Yaeda Chini. 
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na msafara wake, wakikagua ujenzi wa kituo cha polisi Bonde la Yaeda Chini Wilayani Mbulu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...