Na Lydia Churi-Mahakama, Kigoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Serikali kuishirikisha Mahakama ya Tanzania kwenye mipango yake ya uanzishaji wa maeneo mapya ya kiutawala ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake mjini Kigoma, Jaji Mkuu amesema mipango ya Serikali ya uanzishwaji wa wilaya au mikoa izingatie pia uanzishwaji wa Mahakama. Aliongeza kuwa Mikoa na wilaya mpya ndizo zenye ukosefu wa Mahakama hali inayowafanya wananchi kufuata mbali huduma za kimahakama.
Alisema Mahakama kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16 hadi 2019/20) imejipanga kutatua tatizo la ukosefu wa huduma za Mahakama pamoja na kusogeza huduma hizo karibu Zaidi na wananchi. Kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, tayari imeanza ujenzi wa Mahakama tano za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Manyara pamoja na ujenzi wa Mahakama 16 za wilaya na Mahakama Kuu mbili katika Mikoa ya Kigoma na Mara.
Jaji Prof. Juma amesema kupitia ziara yake ya siku saba kwenye Mahakama Kuu kanda ya Tabora amebaini kuwa watanzania wengi hufuata mbali huduma za Mahakama na maeneo mengine ni kutokana na jiografia ya maeneo hayo. Akitolea mfano wa wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Jaji Mkuu amesema kutokana na wilaya hiyo kuzunguka mkoa, wananchi wake hulazimika kufuata huduma za Mahakama Kuu zilizopo umbali wa Zaidi ya kilometa 377.
Jaji mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa pamoja na
wakandarasi wa kampuni ya Masasi Contruction Ltd wanaojenga jengo la
mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma. mahakama ya Tanzania inajenga
jengo hili pamoja na mengine nchini ili kusogeza huduma za mahakama
karibu zaidi na wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...