Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameziagiza Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha zinatekeleza agizo la uanzishwaji wa viwanda 100 na hadi mwezi Septemba mwaka huu viwe vimekamilika.
Mnyeti akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, alisema kila halmashauri ya mkoa huo wenye halmashauri saba, inapaswa iwe na viwanda 15. Mnyeti alisema serikali ilitoa agizo la kila mkoa uanzishe viwanda 100 hivyo na mkoa wa Manyara nao unapaswa kuhakikisha unatekeleza agizo hilo kwa kila halmashauri kuwa na viwanda 15.
Alisema agizo hilo linatakiwa kutekelezwa kwa kila sekta ikiwemo kilimo na mifugo ambazo ndizo shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi wengi wa mkoa huo. “Watumishi wa umma wanapaswa kutambua kila taaluma waliyoisomea wanapaswa kuwekeza kwenye fikra ya viwanda kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa sekta hiyo,” alisema Mnyeti.
Aliwapongeza mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hamis Malinga kwa kutekeleza agizo hilo la uanzishwaji wa viwanda vipya. “Kwenye miezi mitatu iliyopita Halmashauri ya Babati mlikuwa mmeshafanikisha uanzishwaji wa viwanda nane na hadi kufikia mwezi Septemba mtakuwa mmekamilisha viwanda 15 hongereni sana,” alisema Mnyeti. Mkuu wa wilaya ya Babati, mhandisi Raymond Mushi alisema wananchi wa eneo hilo ni wachapakazi wazuri na hujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, wakiwemo maofisa tarafa, madiwani, watendaji wa kata, vijiji, walimu na wenyeviti wa vijiji, juu ya kufanya kazi kwa uadilifu na kutumikia jamii, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi.

Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Mhandisi Raymond Mushi akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga juu ya kufanya kazi na kuwahusia kuwa siku mbili ambazo mtu hawezi kufanya chochote ni jana na kesho hivyo waitumie siku ya leo kwa kutimiza wajibu wao, kulia ni Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Nicodemus Tarmo.

Mkuu wa Wilaya ya Babati Vijijini Mkoani Manyara, Vrajilal Jituson, akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yao ikiwemo suala la elimu.

Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Esta Mahawe akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambapo alijitoa mashuka 10 kwa ajili ya wagonjwa watakaotumia kwenye zahanati ya kijiji hicho iliyozinduliwa na Mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...