Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imechangia kiasi cha Shilingi Milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya Kompyuta katika shule ya Sekondari Misitu iliyopo Wilaya ya Ilala, jijini Da es Salaam.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere, ametoa mchango huo ikiwa ni sehemu ya kuchangia maendeleo kwa jamii alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 9 ya kidato cha Nne katika shule hiyo ambapo wanafunzi 205 wanaotarajia kuhitimu masomo yao mara baada ya kufanya mtihani wa Taifa mwezi Novemba 2018.
Kamishna Mkuu Bw. Kichere, amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kitachangia ujenzi wa Maabara ya Kompyuta na kuwafanya wanafunzi kujifunza na kuongeza uelewa zaidi wa masuala ya Teknolojia.
“Nimesikia katika changamoto mlizozitaja kuwa mnahitaji jengo la maabara ya kompyuta, uzio pamoja na jengo la utawala na mimi nimeona vyema nichangie ujenzi wa jengo hilo ili wanafunzi wapate kujifunza na kuwa na uelewa wa teknolojia kwani dunia sasa inatumia zaidi teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuleta maendeleo”, alisema Kichere
Aidha, Bw. Kichere aliongeza kuwa, ujenzi na maendeleo ya shule za serikali unatokana na kodi hivyo aliwataka wanafunzi, walimu na wazazi kuwa na utamaduni wa kudai risiti za mashine za kielektroniki (EFD) ili kuchangia Mapato yatakayotumika kuboresha ujenzi na uboreshaji wa shule pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii.
Bw. Kichere alisisitiza kuwa matunda ya kodi zinazopatikana pia hutumika kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile ununuzi wa vitabu kwa ajili ya maktaba, utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, ujenzi wa madarasa, mabweni, nyumba za walimu na ununuzi wa vifaa vya maabara na kufundishia.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye
skafu) akimkabidhi cheti mwanafunzi bora katika masomo yote wa kidato
cha nne katika shule ya Sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es
Salaam, Richard Sagwe wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere
akiwahutubia Wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya Sekondari Misitu
iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya kidato cha nne
shuleni hapo.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye
skafu) akiangalia baadhi ya kazi mbalimbali za Sanaa zinazofanywa na
Wanafunzi katika shule ya sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es
Salaam wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye
skafu) akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
wa TRA, Bw. Richard Kayombo (kushoto) pamoja na uongozi wa shule ya
sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali
ya kidato cha nne shuleni hapo.
(PICHA ZOTE NA TRA)KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...