Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Dkt.
Doroth Gwajima akiangalia mtoto ambaye amezaliwa katika Hospitali ya Rufaa
Mbeya Kitengo cha Wazazi Meta. Baadhi ya wajumbe wa Bodi na Maofisa wa
NHIF walitembelea hospitali hiyo kuangalia huduma za wanazopata wanachama
wake.
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya (NHIF), umetembelea Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya na baadhi ya Vituo
mkoani humo kwa lengo la kuangalia huduma wanazopata wanachama wake.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa NHIF ulikutana na Uongozi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya,
Kitengo cha Wazazi Meta na Hospitali ya Uyole ambapo pamoja na mambo mengine
walijadili juu ya huduma zinazotolewa kwa wanachama wa Mfuko.
Akiongoza ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bwana Tryphon
Rutazamba alisema kuwa mbali na kujadili huduma lakini pia wamepata fursa ya
kukagua mradi wa Jengo la Wodi ya Daraja la Kwanza inayojengwa pamoja na
uzalishaji wa Maji tiba katika hospitali ya Rufaa Mbeya kwa fedha za Mkopo wa NHIF.
“Tumepita na kuangalia maeneo ambayo wanachama wetu wanapata huduma,
tumeona pia wanachama na kuzungumza nao ambao wamekiri kupata huduma nzuri
hivyo tunawapongeza hawa watoa huduma kwa jitihada kubwa za uboreshaji wa
huduma ambazo wanazifanya,” alisems Bw. Rutazamba.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya Dkt. Fred Mbwanji
aliushukuru Mfuko kwa kuboresha huduma zake lakini pia kwa fursa ya mikopo nafuu
ambayo imewawezesha kuboresha kwa kiwango cha juu huduma za matibabu
hospitalini hapo.
“Tunajenga Wodi ya Daraja la Kwanza kwa fedha ambazo ni mkopo nafuu kabisa
kutoka NHIF, lakini pia tuna mradi wa kuzalisha Maji Tiba ambao ni mkopo pia kutoka
kwenye Mfuko hivyo unaweza ukaona ni kwa namna gani NHIF imekuwa ni nguzo
kubwa katika uimarishaji na uboreshaji wa huduma,” alisema Dkt. Mbwanji.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi Tryphon Rutazamba akimsalimia Mama na mtoto
ambao ni wanachama wa Mfuko waliokuwa wamelazwa katika Hosptali ya
Wazazi Meta, Mbeya.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Uyole Mbeya Dkt. Sijabaja akitoa maelezo kwa
huduma anazotoa katika hospitali hiyo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...