MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umetoa kauli na kulaani vitendo vya udanganyifu kwenye Shule za Msingi nchini, vilivyofanywa na baadhi ya watendaji wa elimu hadi kusababisha Baraza la Mitihani Tanzania kufuta matokeo ya Darasa la Saba kwa baadhi ya shule.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Bi. Cathleen Sekwao alisema kitendo kilichofanywa na watendaji hao waliopewa dhamana ya kusimamia elimu ni sawa na kuhujumu juhudi kubwa za Serikali na wadau wengine wa elimu zinazofanyika kuinua kiwango cha elimu nchini.

Alisema kitendo cha wanafunzi hao kufutiwa matokeo ya mitihani kimewaathiri wanafunzi kisaikolojia na hisia na kuwapotezea uwezo wao wa kujiamini katika kufanya mitihani mingine, licha ya kwamba walioshirikishwa hawakuwa na uwezo wa kupinga wanachoelekezwa na walimu au viongozi katika jambo hilo.

“Ikumbukwe kuwa mtoto wa Darasa la Saba hana uwezo wa kupinga anachoelekezwa na viongozi au walimu wake hivyo huamini kila anachoambiwa afanye ni chema bila kujua madhara yake ya baadae. Ni dhahiri kuwa kitendo cha kufutiwa matokeo ya mitihani kimewaathiri watoto hao kisaikolojia na kihisia na hivyo kuwapotezea uwezo wao wa kujiamini katika kufanya mitihani mingine na safari yao ndefu ya kutimiza ndoto zao,” alisema Bi. Sekwao.

Alipongeza uamuzi uliofanywa na Serikali kupitia Baraza la Mitihani kuwafanya warudie mitihani ni jambo jema, inaonesha dhahiri kwamba kuna nia ya kuwapa fursa watoto hao. Pamoja na hayo alishauri muda uliotolewa wa kurudia mitihani hiyo ni mdogo kuwawezesha watoto hao kujiandaa na kujijenga kisaikolojia ili kuwa tayari kufanya mtihani mwingine.

“…Tunapendekeza kuwa angalau wapewe mwezi mmoja wa kujiandaa na kujengwa kisaikolojia…Mtandao unaipongeza Serikali kwa kuweza kubaini kitendo hiki cha hujuma na kuchukua hatua za awali. Ni matarajio yetu kuwa uchunguzi utakapokamilika wale wote waliohusika watachukuliwa hatua stahiki za kisheria na kinidhamu ili iwe fundisho kwa umma,” alisisitiza Bi. Sekwao.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Cathleen Sekwao (kushoto) akitoa kauli ya mtandao huo kupongeza Serikali kupitia Baraza la Mitihani kufuta matokeo ya darasa la saba kwa baadhi ya shule kwa ile kuonekana uwepo wa mchezo mchafu kuchezea mitihani hiyo. Kulia ni Meneja Programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met), Bw.Nicodemus Shauri Eatlawe. 

Meneja Programu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met), Bw.Nicodemus  Shauri Eatlawe (kulia) akitoa ufafanuzi kwa wanahabari kuhusiana na kauli ya mtandao huo juu ya kufutwa kwa matokeo ya mitiani darasa la saba. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa REPSSI nchini Tanzania, Edwick Mapalala na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Cathleen Sekwao wakifuaatilia.

Mkurugenzi wa REPSSI nchini Tanzania, Edwick Mapalala (kushoto) akizungumza kwenye mkutano huo wa TEN/MET na waandishi wa habari. Kulia ni Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Cathleen Sekwao akifuatilia. 

Afisa Programu wa TenMet, Bi. Alistidia Kamugisha (kushoto) akichangia hoja katika mkutano huo na wanahabari. Kulia ni Bi. Edwick Mapalala. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...