*Akuta baadhi ya wakandarasi wanasuasua, wengine wako vizuri
*Aitisha kikao cha Mawaziri, Makatibu Wakuu wote kesho saa 5 asubuhi
*Ataka leo jioni apewe taarifa ya kila taasisi inayohusika Ihumwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa eneo la Mji wa Serikali lililoko Ihumwa na kubaini kuwa baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi inayotarajiwa na Serikali.

Waziri Mkuu ameamua kuitisha kikao cha Mawaziri wote na makatibu wakuu wote kesho (Ijumaa) saa 5 asubuhi ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini.Ametoa agizo kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Desemba 27, 2018) mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Mtumba lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

“Nimekagua maeneo yote na kukuta baadhi ya wakandarasi wanatakiwa kujenga majengo ya wizara nne hadi tano. Sijaridhika na baadhi ya kazi, nimeitisha kikao cha Mawaziri wote kesho ili tuangalie ni mkandarasi yupi anaweza kumudu hii kazi.”

“Nimebaini kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama kokoto, nondo, matofali na kikao cha kesho kitahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa Mkoa na Jiji la Dodoma, wakandarasi wote ili tukubaliane kazi hii inaisha lini,” amesema.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma ramani ya Mji wa Serikali wakati alipokagua Ujenzi wa mji huo, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Afisa Mipango Miji katika jiji la Dodoma, William Alfayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi na Kulia ni Katibu  wa Kikosi Kazi cha  Kuhamishia Shughuli za Serikali jijini Dodoma, Meshack Bandawe. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Katibu  wa Kikosi Kazi cha  Kuhamishia Shughuli za Serikali jijini Dodoma, Meshack Bandawe kuhusu Ujenzi wa Mji wa Serikali wakati alipokagua Ujenzi huo, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua Ujenzi wa jengo Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati alipokagua Ujenzi wa Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kazi ya kusuka nondo  kwa ajili ya nguzo za jengo la Ofisi za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati alipokagua Ujenzi wa Mji wa Serikali, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018.  Kulia kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu,  Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua Ujenzi wa Msingi  wa jengo la Ofisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakati alipokagua Ujenzi wa Mji wa Serikali, eneo la Ihumwa jijini Dodoma, Desemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...