Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Digital Opportunity Trust (DOT), Eliguard Dawson (kushoto) akiwa na Naibu Kiongozi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Ubunifu (HDIF), Joseph Manirakiza wakati wakielezea kuhusu kanuni za kidijitali katika miradi ya maendeleo.
Naibu Kiongozi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Ubunifu (HDIF), Joseph
Manirakiza (kulia) akielezea kuhusu kanuni za kidijitali kwa Mkurugenzi
wa Shirika lisilo la Kiserikali la Digital Opportunity Trust (DOT),
Eliguard Dawson. Katikati ni Mtaalamu wa mawasiliano wa HDIF, Hannah
Mwandoloma.
Na Karama Kenyunko
TANZANIA kama zilivyo nchi nyingine za Bara la Afrika, imekuwa ikipiga hatua kubwa katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufikia uchumi wake.
Katika Sera ya Tehama ya mwaka 2016, inaonesha kuwa watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka 17,263,523 mwaka 2014 kufikia 39,808,419 mwaka 2015.
Kutokana na matumizi makubwa ya huduma za mawasiliano, imesaidia sekta hiyo ya mawasiliano kukua kwa kasi kutoka asilimia 8.0 mwaka 2014 hadi asilimia 12.1, mwaka 2015.
Huenda pia haufahamu kwamba, katika ripoti ya Tehama ya mwaka 2014 inaonesha kuwa Tanzania ilipanda nafasi mbili kwa kupata alama 3.04 chini ya alama saba zinazotumika kama kigezo cha kupata ubora duniani.
Hivi sasa, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta hiyo ya teknolojia kwa kuwa vijana wengi wamekuwa wakianzisha miradi ya maendeleo inayofanyika kwa njia ya kidijitali.
Lakini, suala ambalo halifahamiki kwa watu wengi wenye taasisi binafsi, serikali na mtu mmoja mmoja ambao ni wadau wa maendeleo, ni kwamba ili kuongeza ubora katika sekta hiyo ya teknolojia zipo kanuni za kidijitali ambazo unaweza kuzitumia na zikaleta mafanikio makubwa zaidi.
Akielezea kuhusu kanuni hizo na namna zinavyotumika, Naibu Kiongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Ubunifu (HDIF), Joseph Manirakiza anasema wamekuwa wakifadhili mashirika mbalimbali kutekeleza miradi ya kibunifu.
Manirakiza anasema zipo kanuni za kidijitali ambazo zimetengenezwa na wadau wa maendeleo na wanaotekeleza miradi ya kibunifu ili kusaidia katika utekelezaji wa miradi hiyo katika kukuza uchumi na teknolojia.
Kanuni hizo za kidijitali zipo nane ikiwemo kuelewa mazingira ya kuanzishia mradi kwa kutambua mfumo wake, vifaa gani vya kidijitali vinatakiwa kutumika katika eneo husika kama nchi, mkoa au vijiji.
Kanuni nyingine ni kuangalia wingi wa watu katika eneo husika ikiwa ni pamoja na kuandaa bajeti kwa ajili ya masuala ya usalama.
Pia, kujenga mifumo imara ya program kwa kutumia vifaa vya kidijitali kwa kuwa ni muhimu katika kuwaleta watumiaji na wadau pamoja na kuongeza matokeo chanya katika mipango ya muda mrefu.
Vilevile, kabla ya kuanza mradi, unapaswa kukusanya data kutoka kwa watoa taarifa makini wa eneo husika na baadae uzitumie kwa ajili ya kukamilisha mradi.
Ili mradi wa maendeleo uweze kufanikiwa unapaswa kuongeza ushirikiano na watumiaji wako wa mradi ili kuongeza uwanda mpana wa kupata data, ubunifu na vyanzo mbalimbali.
Aidha, kuimarisha mradi kwa kuufanya wa jumuiya kuliko taasisi, kuhakikisha usalama wa taarifa ulizokusanya, namna ya kuzitumia, utunzaji na kuzisambaza.
Pia, kuongeza ushirikiano na jamii au wadau kwa kubadilishana taarifa, mawazo, mikakati na rasilimali zinazozunguka mradi huo, taasisi au sekta husika.
Kutokana na kanuni hizo, Manirakiza anafafanua kuwa miradi mingi iliyoanzishwa haifikii malengo kutokana na kutotumia kanuni hizo na kwamba mpaka sasa mashirika zaidi ya 100 duniani wanazitumia.
"Moja ya kanuni za kidijitali zinaelekeza kuwa ni lazima taasisi za serikali, binafsi na mtu mmoja mmoja zinapaswa kuwafikiria watumiaji wake pindi unapotaka kuanzisha mradi wa maendeleo," anasema Manirakiza.
Anaelezea kuwa kanuni nyingine ni kuelewa mazingira ya unapokwenda kutekeleza mradi kwa kuelewa je kuna watu wanatekeleza mradi unaofanana na wa kwako, watumiaji wangapi na mazingira ya kisiasa katika upokeaji wa miradi hiyo kwa ajili ya kuleta manufaa.
"Miongoni mwa mashirika tuliyoyafadhili na ambayo yameanza kutumia kanuni hizi na wamepata mafanikio makubwa katika miradi yao ni Shirika lisilo la Kiserikali la Digital Opportunity Trust (DOT) lenye lengo la kusaidia vijana kupata ujuzi," anasisitiza.
Pia anasema pamoja na kufadhili, wanaendelea kutoka mafunzo kwa mashirika na wadau wa maendeleo ili kuongeza uelewa juu ya matumizi ya kanuni za kidijitali katika miradi.
Manirakiza anaeleza elimu ya matumizi ya kanuni hizi kwa kupitia mashirika yaliyoendelea zaidi yatasaidia kuamsha ari kwa watu wengine kuweza kuzitumia na kufanikisha miradi yao.
"Ni lazima utumie muda kupanga mradi wako utaufanikishaje kabla ya kuanza utekelezaji kwa sababu kuna maeneo mengine hauwezi kusema unaenda na kompyuta bila kujua eneo unalokwenda kufanyia kazi lina umeme au la," anaongeza Manirakiza.
Hata hivyo, Kiongozi huyo wa HDIF, anasema matumizi ya kanuni za kidijitali yanasaidia kupata faida katika miradi mbalimbali na kwamba huu ni wakati wa kuanza kuzitumia kwa ajili ya kujiendeleza na kuleta maendeleo chanya kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Akielezea mafanikio ya kutumia kanuni za kidijitali, Mkurugenzi wa DOT, Eliguard Dawson anasema kuwa shirika hilo linawasaidia vijana wajasiriamali na waliovyuoni kupata ujuzi wa kazi utakaowasakdia watakapohitajika katika kampuni binafsi na serikali.
Anasema kuwa wamekuwa wakiwashauri vijana hao ili kufikia mafanikio na kwamba wamekuwa wakifanya program mbalimbali na vyuo mbalimbali ikiwemo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA-Pwani) .
Dawson anasema awali DOT hawakuzifahamu kanuni za kidijitali kwa ajili ya miradi kama waliyoanzisha lakini baadae waliangalia namna ya kuzitumia na kwamba zimewaletea mafanikio.
"Tuliangalia ni watu gani wanatoa mafunzo kama tunayotoa sisi katika vyuo vya ufundi, vifaa vya kidijitali wanavyotumia kufundishia na sehemu ya kutolea mafunzo. Lakini tulikumbana na changamoto katika Chuo cha Veta Pwani kwani hawakuwa na vifaa vyovyote vya Tehama na wala haijaunganishwa na mtandao wa intaneti" anaeleza Dawson.
Anaongeza kuwa "Tuliangalia kanuni hizi na baadae tukarudi tena Veta kuangalia namna ya kufanya maboresho ili mradi wetu ufanikiwe ndipo tuligundua kuwa walimu walikuwa wanatumia simu za mkononi zenye uwezo wa kutumia mtandao wa intaneti hivyo tukaamua kuanza kutumia kuwasiliana kwa simu hizo kama sehemu ya teknolojia badala ya kompyuta kwa njia ya barua pepe na kufanya utafiti kwa kutumia simu."
Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa, kwa kutumia kanuni hizo waliona ni rahisi kutatua changamoto walizokuwa wakikumbana nazo katika sekta hiyo ya teknolojia.
Kwa mujibu wa Dawson, teknolojia inakua kwa kasi hivyo kila shule inapaswa watoe mafunzo ya Tehama kwa wanafunzi na walimu.
Anasema ili kufikia malengo ni lazima shule ziwe na miundombinu ya umeme na kama gridi ya Taifa haijapita eneo hilo, matumizi ya nishati ya jua unapaswa kutumika ili miradi ya teknolojia ipate kufanikiwa.
"Huduma ya intaneti katika shule zetu pia inapaswa kupewa kipaumbele kwani hivi sasa watanzania wengi wanatumia simu hivyo waangalie namna ya kuzitumia kwa ajili ya kuelekeza watu watumie kanuni za kidijitali kwa njia ya simu," anasisitiza.
Pia anasema vyuo vinauwezo wa kutumia teknolojia kuandaa miradi ya maendeleo kwa kutumia simu mara baada ya kufahamu mazingira ya kuweka mradi.
Hata hivyo, walimu waliopata mafunzo ya teknolojia wamepewa jukumu la kuwaelekeza walimu wenzao.
Katika kanuni ya watu gani washirikishe, DOT iliwashirikisha uongozi wa chuo cha Veta, walimu, maofisa tawala na kuwaeleza umuhimu wa program hiyo na kwamba wanaamini walimu waliopata mafunzo hayo watasaidia ukuaji wa teknolojia nchini.
"Tumesaidia chuo hiki kupata vifaa vya Tehama na huduma ya mtandao ya Wi-Fi. Mpaka sasa mradi wetu umesaidia watu kujiendeleza kikazi na kubadilish mfumo wa awali," anafafanua.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Veta na kwamba wanampango wa kuanzisha mafunzo ya teknolojia Chuo cha Veta Chang'ombe Dar es Salaam.
Anatoa wito kwa serikali kwamba sera ya elimu inayoelekeza kila Wilaya kuwa na chuo cha ufundi sio mbaya lakini itakumbana na changamoto kwa kuwa wafadhili wengi wanaangalia kuwekeza katika kutoa elimu.
Hivyo, anasema sera hiyo inapaswa kuangaliwa upya kwa kuboresha majengo yaliyopo kutoa elimu kwa watu wengi zaidi.
Diwason anasema katika uanzishaji wa miradi ni jambo la msingi kufanya utafiti kabla ya kuanza mradi wowote wa kidijitali ili kusaidia mradi kuwa wa manufaa.
"Kwa kuwa vijana wengi wanatengeneza miradi katika njia za teknohama wanatakiwa kuwashirikisha watumiaji wa teknolojia husika kwani mradi wa kutoa mafunzo Veta ingekuwa rahisi kukamilika endapo wangezifahamu kanuni kwa sababu kupitia utafiti wangetambua kuwa hawakuwa na vifaa vya teknolojia," anasisitiza Dawson.
Ni dhahiri kuwa kila mwenye lengo la kukua kimaendeleo na kiuchumi anapaswa kuzifahamu kanuni hizi kwa sababu miradi mingi imefanikiwa kama ilivyo kwa DOT




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...