Ruge Mutahaba.
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MAISHA
yangu ya uandishi wa habari kwa miaka 19 sasa, hakuna siku hata moja
nimewahi kuandika makala, maelezo, maoni au ushauri kuhusu Mtanzania
ambaye anasumbuliwa na maradhi.
Nimekuwa
na utamaduni wa kutoa pole au kushiriki kwenye maombi ya kuhakikisha
mwenzetu anayeumwa, Mwenyezi Mungu ampe unafuu na apone haraka. Nimekuwa
nikifanya hivyo kadiri ninapopata taarifa. Ila sijawaji kuandika
maelezo mareeefu kumzungumzia mgonjwa!
Kwa
mara ya kwanza leo naomba nivunje mwiko huo. Iwapo nitakuwa nakosea
naomba nisamehewe. Nimeshindwa kuvumilia, nimeshindwa kukaa kimya.
Nimeshindwa kuzungumza na moyo wangu na kisha kubaki nayo kichwani.
Hapana nimeshindwa. Naomba ruhusa niandike kuhusu Ruge Mutahaba.
Ndio!
Nataka kumzunguzia Ruge Mutahaba. Huyu huyu Bosi Ruge, ni huyu huyu
Ruge ambaye wengi wamefanikiwa kupitia kwenye mikono yake. Ruge ambaye
ukisikia atazungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari vya Clouds
Media Group wote tunasubiri. Tunaka kufahamu anazungumza kuhusu nini.
Ruge ambaye tunamuita Scofield wa Tanzania.
Mungu
Muumba wa mbingu na ardhi, nipe ujasiri wa kuandika maelezo ambayo
yatanyooka na kueleweka kwa haraka. Unapotaka kumzungumzia Ruge Mutahaba
lazima kichwa kitulie, lazima uwe na hakika ya kile ambacho unataka
kukisema.
Najua
na Watanzania wanajua kwa sasa Bosi Ruge yupo kitandani. Ruge anaumwa.
Pole kaka. Natoa pole kwako bosi Ruge. Nina hakika Mungu atakunyanyua na
kusimama tena. Mungu atakuponya, Watanzania kila mmoja kwa imani yake
wanakuombea Ruge upone haraka. Pole kaka, pole rafiki, pole swahiba wa
Watanzania.
Taarifa
za kuumwa kwako nimezipata kupitia taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa
zikitolewa kuhusu wewe. Sebastian Maganga alitoa taarifa rasmi kuhusu
kuumwa kwako.
Na
juzi hapa nimemsikia mdogo wako Mbaki Mutahaba, aliyetoa maelezo kuhusu
hali yako. Nimemsikia akitoa taarifa ya gharama ya fedha ambayo
inatumika kila siku kwa ajili ya matibababu yako.
Ruge
narudia tena, sina shaka hata kidogo, afya yako itaimarika na kurejea
kwenye majukumu yako ya kila siku. Nikiri sijawahi kukutana na wewe
'Live' tukazungumza au kujadili chochote. Huo ndio ukweli. Hata hivyo
kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano, nimekuwa nikikutana na
wewe kupitia vyombo vya habari mbalimbali na hasa vile ambavyo
unavisimamia vya Clouds Media Group.
Kaka
kupitia wewe umenibadilisha kwenye mambo mengi. Umenifundisha maisha ni
nini? Ili uishi unatakiwa kufanya nini? Unatakiwa kufanya mambo ya aina
gani kufikia mafanikio. Ruge Mutahaba pole kaka. Katika maisha kuna
watu ambao najua umekutana nao na kuzungumza nao.
Najua
ni wengi lakini idadi yao haizidi wale ambao umewafikia kupitia vyombo
vya habari. Sitaki kuzungumzia wasanii wa fani mbalimbali. Sisemi
uliokutana nao kwenye jukwaa la fursa ambalo huambatana na tamasha la
Fiesta.
Ruge
wewe ni mwalimu wa kila kitu. Mwenyezi Mungu aliamua kuweka vitu ndani
yako kwa ajili ya wengine. Leo unaumwa, mioyo yetu inaumizwa na kuumwa
kwako. Pona kaka. Tunaumia kwa sababu kukosekana kwako katika kipindi
hiki yapo baadhi ya mambo hayaendi sawa. Kuna kitu tunaona kinakosekana.
Tunamuomba Mungu akupe afya njema na urejee nyumbani.Tunakuhitaji sana.
Amka
Ruge wetu, amka Bosi Ruge, amka Scofield wa Tanzania. Najua umekaa kwa
muda mrefu kitandani lakini huu ni wakati sahihi kwako kumka
tena.Tunakusubiri kaka, tunakusubiri kaka mkubwa. Njoo tuendelee na
maisha ya kuijenga Tanzania yetu.
Uwezo
wako, maarifa yako, akili yako na ubunifu wako umechangia kwa kiasi
kikubwa nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo. Unaweza usione moja kwa moja
lakini namna ambavyo umetengeneza fursa na Watanzania wakazitumia vema
wengi wao wamebadilika. Wamepiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Muangalie
Nasibu Abdul a.k.a Diamond. Amepita kwenye mikono yako. Wapo wengi
ambao wamenufaika kimaisha kupitia akili yako. Njoo kaka tunakusubiri
nyumbani Tanzania. Kama binadamu najua huwezi kufanya kila kitu
kikafurahisha watu wote lakini ukweli utabaki kuwa wengi wamenufaika
kupitia wewe.
Naandika
huku nikikumbuka ile kauli mbiu 'Fungulia Dunia kuwa unachotoka'. Kaka
Ruge binafsi nimekuwa ninachotaka. Nikwambie kaka Ruge kuumwa kwako,
tunaumwa wengi. Huo ndio ukweli.
Mungu
amekupa akili ya kujua ufanye nini na kwenye jambo gani. Umekuwa msaada
mkubwa kwa Watanzania wengi. Hakuna kampeni ambayo ulianzisha ikakwama.
Nimekumbuka wimbo wa Tuulinde na Amani ambao uliishirikisha wasanii
mbalimbali.
Kaka
Ruge tumekuzoea kukuona unaumiza kichwa kuhakikisha mambo yanakwenda.
Rudi brother tuijenge nchi yetu. Sioni mahali ambapo Ruge ulitaka kufika
ukakwama. Kila mahali ambako ulitamani kufika ulifanya hivyo.
Ruge
ni wewe ambaye ukiamua jambo liwe linakuwa. Kikubwa zaidi ambacho
najifunza kutoka kwako ni uwezo wako mkubwa wa kuchuja kipi uzungumze
sasa na kipi uzungumze baadaye.
Tanzania
imesimama, inakusuburi uamke kitandani. Inakusubiri urudi. Rudi kaka
Ruge, Rudi Bosi Ruge. Njoo tuungane kwenye harakati za maisha yetu ya
kila siku.
Kukuzungumzia
wewe unaweza kutumia siku, wiki, mwezi na hata mwaka bila kumaliza.
Umefanya mengi na natamani kuona ukiendelea kufanya mengi zaidi. Moyo
wangu unaumia, machozi yanatoka. Ugonjwa wako unatuliza wengi. Amka
ndugu yetu, amka Mzee wa vipaji lukuki.
Nikiri
nimefarijika kuona kuna kampeni maalumu ya kuchangisha fedha kwa ajili
ya kusaidia matibabu yako. Tumeambiwa kwa siku gharama ni kati ya Sh5
mpaka 6 milioni kila siku.

Ruge Mutahaba (kulia) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mh.Paul Makonda
Ni
wakati wetu Watanzania kuungana kuchangia matibabu yako. Ni matumaini
yangu Watanzania tutaendelea kukuombea na kukuchangia kadiri ya uwezo
wetu. Familia kwa nafasi yake imeendelea kutimiza majukumu ya
kuhakikisha mwanafamilia wao anapata matibabu.
Rais Dk. John Magufuli alikuwa wa kwanza kutoa fedha kwa ajili ya matibabu ya Ruge.
Kaka
Ruge siku zote umekuwa mstari wa mbele kuchangia wengine, hivyo nasi
tunayo nafasi ya kukuchangia. Nia yetu ni kuona afya yako inakuwa imara.
Ulitumia nafasi yako kuwashika mkono Watanzania waliopoteza matumaini,
ni wakati wetu nasi kukushika mkono.
Uliwapa
faraja waliokosa faraja, ni wakati wetu kukupa faraja.Tanzania All
Stars uliwatumia mara kwa mara pale ulipoona iko haja ya kusaidia jamii
iliyo kwenye mataabiko. Ni matumaini yangu Tanzania All Stars nao
watakushika mkono.
Kaka
Ruge wewe ni bonge la binadamu. Mungu amekupa utu na ubinadamu. Vyote
unavyo. Nitakuombea kwa Mungu akuponye maradhi yanayokusibu. Nitakuombea
kila sekunde, kila dakika na kila saa.
Nihitimishe
kaka Ruge pole kwa kuumwa. Watanzania tunakuombea. Ukiupata ujumbe huu
naomba utambue bado tunakupenda na tuko pamoja nawe.
Hata
hivyo nikiri tu naumia sana ninaposikia baadhi ya watu wakiwamo wasanii
ambao umewajenga kupitia vyombo vyako vya habari, wakitoa lugha za
kejeli, dharau na kiburi dhidi yako. Inaumiza sana. Nawasikiliza wee
kisha nasema Mungu wahurumie. Bosi Ruge pole. Pole kaka.
Simu: 0713833822.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...