NA YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Wakulima 69 wa kijiji cha ligera wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma
wamepatiwa mafunzo ya siku tatu ya Kupanda mpunga kwa njia ya
Mfereji, kutawanya ,kwa njia ya ibaraki na kwa njia ya shimo ili
kuwewezesha kupata mavuno ya kutosha.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa vitendo na kwa nadharia na wataalamu
wa kilimo kutoka chuo cha kilimo MATI Mtwara waliowafundisha
wakulima njia za upandaji mpunga wa mabondeni na unaotegemea mvua.
Aidha wataalamu hao ni Doroth Mushi, Daudi Kasabuku na Kenedy Siame
wote ni wakufunzi kutoka chuo cha kilimo MATI Mtwara ambao
walifundisha namna ya kupanda mpunga aina ya Saro tano,Mtalimawangu na
supermbeya.
Hata hivyo waliwafundisha wakulima hao namna sahihi ya kuvuna
mpunga uliotayari kuvunwa na namna sahihi ya kuuhifadhi mpunga huo
na kisha namna sahihi ya kukoboa mpunga tayari kwa kupelekwa
sokoni.
Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa mpunga kijiji cha ligera
Lukanus Luena alisema watayatumia mafunzo hayo waliyoyapata
kuongeza uzalishaji wa mpunga na kujipatia kipato kwa mwanakikundi
mmoja mmoja na kikundi pia.
Bwana Luena alidai mafunzo hayo yamewaongezea morali ya kulima
zaidi kwa kutumia njia sahihi za kilimo cha kisasa na kuahidi
kuongeza wanachama wengine katika kikundi hicho kutokana na hitaji
la wakulima wengine ambao wameonesha nia ya kujiunga na kikundi hicho
cha wakulima wa mpunga.
Ofisa kilimo anayeshughulikia umwagiliaji Bwana Eleuter Mndendemi
aliwataka wakulima wa kijiji cha Ligera kuyatumia mafunzo hayo
vyema kwa kuonesha matokeo chanya y a mapato yanayoshabahiana na
wakulima wanaolima kwa kitaalamu na kuonesha utofauti na awali
kabla ya kupatiwa mafunzo hayo.
Mafunzo ya kilimo cha mpunga wa Mabondeni ( kutegemea maji ya Mvua)
unafadhiliwa na JICA(Japan International Cooperation Agency) kwa
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo pamoja na chuo cha Kilimo
MATI-Mtwara.
Kikundi cha wakulima wa Mpunga wa kijiji cha Ligera kilianzishwa mwaka
2017 kikiwa na wanachama 30 na mwaka huu 2019 kikundi kina
wanakikundi 80 na kati ya hao waliopatiwa mafunzo ni 69 ikiwa
wanawake 29 na wanaume 40.
Mtaalamu wa kilimo Kenedy Siame (mwenye kofia nyekundu) akiwaelekeza wakulima umuhimu wa kuzingatia vipimo wakati wa upandaji wa mpunga,Picha ya pili wakulima wakiwa katika mafunzo kwa vitendo namna ya kukata mpunga na kuuhifadhi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...