Na Woinde Shizza Michuzi TV, Arusha
Jumla ya vijana 9,339 kutoka vikundi 380 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe, na Mbeya wamenufaika na elimu mbalimbali ikiwemo ya ujasiriamali ambayo imewawezesha kujitambua na kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Aidha vijana hao wamenufaika katika elimu kuhusu akiba na mikopo, utunzaji wa fedha, ujasiliamali na ujuzi tete, mpango biashara na kilimo biashara ambazo kwa pamoja zimewawezesha wao kujitegemea.
Hayo yalisemwa mkoani Arusha katika sherehe za wiki ya unywaji maziwa duniani ambayo kitaifa inafanyika jijini Arusha na Meneja wa kilimo biashara kutoka shirika la Heifer International linaloongoza jitihada za kutokomeza njaa na umaskini ,huku likizingatia kutunza mazingira, Frimina Kavishe wakati akizungumzia jinsi ambavyo wamewezesha vijana katika nyanja mbalimbali katika kujikwamua kiuchumi.
Frimina alisema kuwa, vijana hao wamefikiwa kupitia mradi wa ushirikishwaji vijana katika sekta ya kilimo na mifugo Afrika mashariki (EAYIP) ambapo wamelenga vijana kuanzia umri wa miaka 15-24 kwani ni kundi lililosahaulika Sana na lina vipaji vikubwa ambavyo vinahitaji kuendelezwa .
"mradi huu umeanzishwa kwa ushirikiano na Taasisi ya mastercard ukilenga kuboresha maisha ya vijana nchini Tanzania na Uganda kwa kutengeneza fursa za ajira na ujasiriamali miongoni mwa vijana 25,000 hadi kuisha kwa mradi huo ifikapo mwaka 2021 na unalenga vijana wanaokosa fursa za kiuchumi na mradi huu ulianza tangu oktoba 2016"alisema Frimina.
Aliongeza kuwa, mradi huu una malengo mkakati minne ikiwa ni pamoja na kuwapatia ujuzi na maarifa vijana ili waweze kujiajiri kupitia mnyororo wa dhamani wa maziwa, kuku, mboga mboga na matunda, mahindi, samaki,viazi mviringo na mimea jamii ya mikunde sambamba na kuwaunganisha na taasisi za kifedha, kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia vijana wengi kujiajiri kwenye sekta ya kilimo na mifugo na kudurufu muundo wa vitovu yaani (sehemu za biashara).
Naye Meneja ushirika wa wajasirimali vijana wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe, George Hayuka alisema kuwa, lengo kubwa la mradi huo ni kuongeza kipato kupitia ajira na maendeleo ya kibiashara katika sekta ya kilimo huku ukilenga kuwajengea uwezo vijana katika ujuzi maalumu juu ya kuanzisha biashara ama kupata ajira kupitia shughuli za kilimo.
Hayuka alisema kuwa, mradi huo pia unalenga kuendeleza ama kurudufu muundo wa vitovu katika minyororo mipya ya thamani kama vile kuku, kilimo cha mbogamboga, matunda na mazao ya nafaka na mizizi sambamba na kuongeza ushiriki wa vijana wa kike na wa kiume .
Aliongeza kuwa, baada ya kumalizika kwa mradi huo, shirika hilo wakishirikiana na wafadhili wa taasisi ya mastercard wameanzisha Vitovu 7 kama sehemu ya biashara yaani ushirika wa vijana ambao utakuwa ukiendelea mara baada ya kumalizika kwa mradi huo huku wakiunganishwa na masoko ili wawe na uhakika wa soko la bidhaa zao na kupata huduma mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa Chama kikuu cha wafugaji mkoa wa Songwe, Isaya Mbindi alisema kuwa, shirika hilo limewawezesha wafugaji hao kufuga ngombe wa kisasa sambamba na kupata elimu juu ya uhimilishaji kupitia mradi wa uendelezaji wa sekta ya maziwa Afrika mashariki (EADD).
Mbindi alisema kuwa, kupitia mradi huo wa EADD wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2003 na upo mbioni kumalizika wameweza pia kuanzisha viwanda vidogovidogo ambapo wameweza kujiunga kwenye vyama vya ushirika ambapo wameweza kunufaika zaidi ya wafugaji mia nne kwa mkoa wa Songwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...