Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewataka watoa huduma katika vituo vya afya na hospitali nchi nzima walio katika orodha ya mfuko huo kutowanyanyapaa wanachama wake.
Kauli hiyo imetolewa leo wakati wa kikao kazi kati ya watumishi wa mfuko huo na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kilichofanyika ukumbi wa Idd Nyundo uliopo katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya Wahariri pamoja na kujadili masuala mbalimbali, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga amesema anachofahamu vituo vyote vinavyotoa huduma za afya kwa wateja wa mfuko huo wanaelewa taratibu zilizokuwepo na amesisitiza kila mwanachama anayo haki kupata huduma kulingana na aina ya kadi aliyonayo.
Ameongeza kuwa alishawahi kupokea malalamiko katika baadhi ya hospitali, lakini baada ya kufuatilia kwa sasa kila kitu kipo sawa huku akieleza unajua mfuko wao una wateja wengi, kama wataamua kuacha kufanya kazi hospitali yoyote basi itapoteza watu kwa kiasi kikubwa.
Amesema ndio maana wameweka wazi kwa yeyote anayeonesha kunyanyapaliwa au kutendewa kinyume na taratibu za huduma za kiafya atoe taarifa kwetu tutalishughulikia ndani ya muda mfupi.
Pia Konga amesema lipo tatizo la wizi au ubadhirifu katika baadhi ya watoa huduma. "Mifuko mingi ya bima ya afya duniani inalalamikia wizi unaofanywa kati ya wanachama kudanganya watoa huduma kuwema bili kubwa ya matibabu kinyume na bili halisi au watumishi wasio waaminifu wa NHIF kuuibia mfuko,".
"Zipo kesi nyingi tunazifuatilia kwenye baadhi ya hospitali. Lakini kwa sasa tunafanya utafiti. Tukishajipanga tutalimaliza hili tatizo.Lakini pia lipo tatizo la wanachama kuendelea kuwa na wategemezi waliopitisha umri wa miaka 18. Tunaamini huyo anatakiwa kuwa katika utaratibu mwingine wa uchangiaji. Ndiyo maana tyliamua kupeleka huduma za bima ya afya kwa wanafunzi ambapo wanalipia Sh 50,400 kwa mwaka," amesisitiza Konga.
Awali akiwasilisha mada kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mkurugenzi wa Wanachama wa NHIF, Mbaruku Magawa amesema wamekuwa wakikipa fedha nyingi katika vituo vyote vilivyo kwenye utaratibu wao ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma stahiki.
"Mfano kwa mwaka 2018/19 tumelipa jumla ya Sh Bilioni 339.06 kwa vituo vya afya 7,400 nchini. Hapo zikiwemo hospitaki za mikoa, wilaya, Zahanati na Hospitali ya Taifa," amesema Magawa.
Amebainisha kwamba mfuko huo ulioanzishwa mwaka 2001 kwa Sheria Sura namba 395 umetimiza miaka 18. Ambapo hadi sasa kuna wanachama 16,969,943 sawa na asilimia 32 ya watanzania wote.
Wanajipanga kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanajiunga na mfuko huo ili kupata huduma za afya kwa wakati na gharama nafuu. Hasa ikizingatiwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanaongezeka siku hadi siku.
Akitolea mfano, takwimu za mfuko zinaonyesha mwaka 2014/15 idadi ya wagonjwa waliotibiwa magonjwq yasiyo ya kuambukizwa walikua 286,806.
Na kwamba ndani ya miaka minne idadi imeongezeka maradufu ambapi takwimu za mwaka 2017/18 zinaonyesha kuna wagonjwa 1,574,803 waliotibiwa kupitia NHIF wakisumbuliwa na maradhi yasiyo ya kuambukiza.
Wakati huo huo NHIF imeahidi kuwa karibu na wanachama wake kwa kutoa taarifa za mara kwa mara kupitia vyombo vya habari ikiwemo elimu juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya lakini pia kuzisaidia baadhi ya hospitali zisizo na uwezo wa kuwa na vifaa tiba kwa kuwapa mikopo ili wanachama wao wapate huduma popote ndani ya nchi.
Akitoa shukrani kwa watumishi wa mfuko huo kwa niaba ya wahariri wa vyombo vya habari nchini,Celina Wilson kutoka Gazeti la Uhuru amesema wahariri kupitia kikao hivyo ameongeza uelewa na ufahamu kuhusu mfuko wa Taifa wa Bima ya afya huku akieleza wahariri watahakikisha wanakuwa makini katika kuandika habari za mfuko huo.
"Tunawahakikishia Wahariri tutatumia kalamu zetu na vyombo vyetu vizuri katika kuandika habari zinazohusu afya.Kuna mengi ambayo tumeyafahamu kupitia kikao hiki,kikubwa tuendeleee kushirikiana na wahariri tupo tayari,"amesema Wilson.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Bernard Konga akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini leo jijini Dar es Salaam
Mmoja ya wahariri akizungumza wakati wa kikao kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini na maofisa wa NHIF .Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dar es Salaam
Mhariri kutoka Gazeti la Uhuru Celina Wilson akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya(NHIF) baada ya kufanyika kikao leo jijini Dar es Salaam.

Maofisa wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya wakawa katika picha ya pamoja na Wahariri wa vyombo vya habari nchini
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...