Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Lusubilo Mwakabibi awatahadharisha wakazi wote wa Manispaa na viunga vyake kuchukua tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu .
Alibainisha kuwa kukithiri kwa uchafu katika maeneo mengi ni sababu mojawapo inayopelekea mlipuko wa magonjwa ikiambatana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama iwapo yatatumiwa katika chakula au mtu kunywa bila ya kuchemshwa kwa kiwango kinachohitajika,alibainisha kwamba usafi wa mazingira ni wa msingi zaidi ili kujilinda na magonjwa ya mlipuko.
“Manispaa ya Temeke imejipanga kwa kutoa elimu ya uhamasishaji na tayari wadau wa Afya wameanza kutembelea nyumba kwa nyumba katika maeneo yote yaliyoathirika sambamba na ugawaji wa dawa za usafi ili kuangamiza mazalia”.Alibainisha zaidi
Tangu ugonjwa wa kipindupindu uliporipotiwa kwa Manispa ya Temeke tarehe 20/04/2019 wagonjwa 48 wamehisiwa mpaka sasa, na kati yao vipimo 10 vimeonesha uwepo wa ugonjwa huo na vifo vilivyoripotiwa ni 2 tu.
Nae Mratibu wa ufuatiliaji magonjwa wa Manispaa ya Temeke Prisca Uswege alibainisha kuwa mpaka sasa nyumba 400 zimetembelewa na wakazi 123 wamepatiwa elimu ya namna ya kujikinga na mlipuko huo sambamba na ugawaji wa water guard pamoja na dawa ya Chlorine.
Nae Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke Dr.Gwamaka Mwabulambo alisema “tayari kuna kambi maalumu iliyopo katika Hospitali ya Temeke kwaajili ya magonjwa ya mlipuko ambapo matibabu na uangalizi kwa wagonjwa hao hufanyika kwa urahisi zaidi”.
Dr. Mwabulambo alibainisha zaidi kwamba dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni pamoja na kuharisha mfululizo, kutapika,macho kudidimia ndani, kinyesi na matapishi yenye rangi kama ya maji ya mchele, pamoja na ngozi kusinyaa.
Pamoja na hayo ameeleza namna ya kujikinga na mlipuko huo kwa kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa sabuni kabla ya kuandaa chakula ama kumlisha mtoto,kunawa mikono kwa maji safi na salama baada ya kutoka chooni au kumsafisha mtoto aliyejisaidia,kusafisha matunda ama vyakula vibichi kama matunda na mbogamboga, kuhakikisha unatumia choo kwa usahihi,kula chakula cha moto,kufunika chakula kilichoandaliwa tayari kwa kula,na ukiona mtu anatiririsha au kutapisha choo,toa taarifa haraka kwenye ofisi za serikali ya mtaa au kata zilizokaribu na nawe.
Kipindupindu kitakwisha iwapo mazingira bora ya kukiepuka yatakuwepo huku jamii nzima ikipewa elimu ya namna ya kujilinda na magonjwa ya mlipuko sambamba na kuhaikisha kanuni za Afya zinazingatiwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...