Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
UANDIKISHWAJI wa vijana katika jeshi la kujenga taifa (JKT) unaoendelea katika Mikoa yote nchini na visiwani Zanzibar umeingia dosari baada ya kugubwika na udanganyifu wa hali ya juu hali iliyoilazimu jeshi hilo kutatua changamoto hiyo kwa kupitia upya vijana wote walioandikishwa kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa habari na mawasiliano Luteni Kanali Gaudance Gervas Ilonda amesema kuwa baada ya kutangaza nafasi kwa vijana kwa kujitolea katika jeshi hilo changamoto zimejitokeza katika zoezi la uandikishwaji huku akieleza changamoto mojawapo ni vijana kujiandikisha Mikoa tofauti na ile wanayoishi na hiyo ni shinikizo kutoka kwa wazazi na walezi hali inayosababisha vijana wa Mikoa husika kukosa nafasi hizo ambazo zimetolewa sawa kila sehemu kulingana na maeneo na idadi ya watu.
Pia ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakipeleka majina ya vijana katika makao makuu ya jeshi la kujenga taifa na Mikoani kwa malengo ya kupata nafasi hizo kwa urahisi zaidi huku akieleza kuwa jeshi hilo halitoi ajira bali linawaandaa vijana hao kuwa wazalendo na viongozi bora kwa baadaye.
"Baadhi ya viongozi wamekuwa wakileta majina 10 hadi 20 ya vijana ili waweze kupata nafasi katika jeshi la wananchi, huku ni kujitengenezea kikosi kwa matumizi yao binafsi kwa baadaye jambo ambalo ni kinyume na kanuni za jeshi hilo" ameeleza Luteni Ilonda.
Aidha amesema kuwa changamoto nyingine katika zoezi hili la uandikishwaji ni udanganyifu wa vyeti vya elimu, vyeti vya kuzaliwa kwa kudanganya umri na afya pamoja na utapeli wakati wa uandikishwaji ambapo wazazi na walezi huombwa fedha ili kuweza kupata nafasi hizo.
"Katika baadhi ya maeneo ya uandikishwaji wazazi huombwa fedha ili kupata nafasi katika jeshi la kujenga taifa, kwa jeshi letu hatuna nafasi hizo na atakayebainika ataondoshwa mara moja" amesema Luteni Ilondo.
Vilevile amesema kuwa kufuatia dosari hizo ambazo hawataweza kuzifumbia macho jeshi la kujenga taifa kwa kushirikina na jeshi la wananchi, mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA), Wizara ya elimu, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) pamoja na mamlaka nyingine watashirikiana katika zoezi kabambe la kupitia upya vijana wote walioandikisha kote nchini pamoja na kupitia nyaraka na vyeti vyote kwa lengo la kupata vijana halali, watanzania, wenye afya na wanaotoka maeneo husika ili waweze kuingia katika jeshi hilo na kupata mafunzo ya uzalendo, umoja, weledi, upendo na kujali mali za umma.
Luteni Ilonda amesema kuwa kwa watakaobainika wameshiriki katika udanganyifu huo kwa namna yoyote ile watakamatwa na kufunguliwa mashtaka na hakuna atakaye fumbiwa macho na hata wale waliotumia dhamana vibaya hawatastahimiliwa.
Mwisho amewataka wananchi kufuata taratibu za uombaji wa nafasi hizo ambazo sifa za kujiunga zimebandikwa katika maeneo ya Wilaya na ofisi husika huku akiwataka vijana wanaojiunga na jeshi kuelewa kuwa hiyo sio tiketi ya ajira jeshini au serikalini bali ni sehemu ya kujifunza uzalendo na kuwa viongozi Bora wa baadaye.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...