ZOEZI la usajili kuelekea mashindano ya mbio za riadha ya John Stephen Akhwari International Marathoni limeanza huku mbio hizo zikitarajiwa kufanyika Juni 9 mwaka huu.
Mbio hizo za wazi za kilomita 21,kilomita 5 na km 2 ambazo zitafanyika katika uwanja wa Kumbu kumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini hapa zinatarajiwa kushirikisha zaidi ya wanariadha 1500 kutoka ndani na nje ya nchi .
Mkurugenzi wa mbio hizo Sylvester Orao ameliambia Championi ijumaa kuwa zoezi la usajili limeanza katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa na kuwaomba wanariadha wote wanaotarajia kushiriki wafike kujiandikisha tayari kabisa kwa mbio hizo na kuongeza kuwa garama uandikishaji ni shilingi elfu kumi na tano.
“ Ndio mara ya kwanza mbio zetu kufanyika naamini zitapata uzoefu mkubwa lakini pia wapo wadhamini ambao wametuunga mkono mpaka sasa kuhakikisha mbio hizi zinafanyika kwa ubora uliokusudiwa,”alisema Orao.
Alisema tayari washiriki kutoka nje ya nchi wameanza kujiandikisha kwa njia ya mtandao ikiwa ni kutoka katika nchi za Kenya Cameroon,Nigeria,Uholanzi ,Marekani na Uingereza huku washiriki kutoka ndani ya nchi mikoa ya Morogoro,Mtwara,Dar es salaam,Tanga,Kilimanjaro na Manyara pia wamethibitisha kushiriki.
Zawadi kwa washindi wa kilomita 21 kwa wanawake na wanaume ,mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi laki nane,mshindi wa pili atapata laki sita na mshindi wa tatu atajinyakulia shilingi laki nne huku mshindi wa nne hadi wa kumi zawadi za fedha pia zitatolewa.
Mbali na zawadi kwa washindi wa km 21 pia washindi wa km 5 kuanzia namba moja hadi sita atapata fedha taslimu,huku medali za dhahabu zikitolewa kwa wale watakaokimbia km 21,shaba kwa km 5 pia vyeti vya uthibisho wa ushiriki utatolewa.
Akizungumzia suala la vibali kwa wanariadha watokao nje ya nchi liko pale pale kwani hata shirikisho la Riadha nchini(RT) linahimiza wote wanaotoka nje ya nchi waje na vibali kutoka katika vyama vyao ili waweze kushiriki.
Alisema lengo la mashindano ni kumunzi mwanariadha wa zamani alieiletea Tanzania heshima mwaka 1968 katika mashindano ya Olimpiki ya Mexico mzee John Stephen Akhwari ambae licha ya kuumia mguu katika mashindano hayo lakini alipambana na kumaliza mbio na kufanikiwa kuweka historia katika mashindano ya Olimpiki
picha maktaba mwanariadha wa kimataifa John Stephen Akhwari akiwa ameshika baadhi za medali alizoshinda kipindi alipokuwa akikimbia akishiriki mbio mbalimbali
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...