Na Moshy Kiyungi,Tabora.
Japokuwa imepita miaka 13, tangu TX Moshi William alipofariki dunia, hadi leo kumbukumbu hazijatoweka vichwani mwa wapenzi na washabiki wa mwanamuziki huyo.
Tungo zake zilizokuwa zimejaa maudhui mema kwa jamii, zilimuongezea sifa kemkem katika kipindi chote maisha yake katika muziki.
TX Moshi William alizaliwa Korogwe mkoani Tanga mwaka 1958, akapewa jina la Shaban Ally Mhoja Kishiwa, baadaye alikuja kubadilisaha akawa Moshi William.
Alivunjika mguu katika ajali ya gari baada ya kupata ajali ya gari lililoparamia mti wa Mvinje pale Mivinjeni, barabara ya Kilwa jijjini Desemba 16, 2005 iliyompelekea kuvunjika mguu.
Februari 13, 2006 akalazwa katika hospitali ya Burere iliyoko Kibaha mkoani Pwani.Siku zilivyokuwa zikisonga mbele, mguu huo kuanza kumsumbua kwa kutunga usaha, akahamishiwa katika Hospitali ya Regency Machi 15, 2006 baada ya kugundulika kuwa pia alikuwa na matatizo ya figo.
Matatizo yalipoendelea Machi 18, 2006 alihamishiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye kitengo cha kushughulikia mifupa MOI.
Kwa mapenzi ya Mungu TX Moshi William aliaga dunia Machi 29, 2006 katika hospitali hiyo ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.Baada ya kifo hicho mwili wake ulishushwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi yaliyoko maeneo ya Keko Machungwa, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mjane wa mwanamuziki huyo, Bi Asha Seif, alisema chanzo cha kifo cha mumewe kilitokana na kadhia ya mguu pamoja na figo.
Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa bendi hiyo Dk. Saidi Mabera, Moshi William maarufu kwa jina la TX alijiunga na bendi ya Juwata mwaka 1982, akitokea katika bendi ya Polisi Jazz.
Mwanamuziki huyo alijipatia umarufu mkubwa kwa kutunga nyimbo zilizokuwa na mafunzo katika jamii. Baadhi yake ni kama Ashibae, Mwaka wa Watoto, Msafiri Kakiri, Asha Mwanaseifu, Kaza Moyo, Ajuza, Ndoa Ndoano, Mwanamkiwa, Ajali, Nyongo mkaa na Ini, Isihaka Kibene, Harusi ya Kibene, Piga Ua Talaka Utatoa na nyimbo nyingine nyingi.
Moshi William hadi mauti yalipomfika, tayari alikuwa amefanikwa kurekodi albamu takriban 13
Baadhi ya wapenzi wa muziki wa dansi katika miji mbalimbali ya Afrika Mashariki na Kati, walikuwa wakimfananisha sana na marehemu Madilu System, aliyekuwa mwanamuziki toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kutokana na mitindo ya unyoaji wa nywele, uvaaji hadi namna ya ya uimbaji.
Kifo cha mwanamuziki Moshi William kiliacha pengo kubwa katika ulimwengu wa muziki wa dansi, ikizingatiwa sauti yake iliyokuwa ya kuvutia, akitunga nyimbo zenye hisia kali zilitokana na maswahibu ya maisha yake.
Wanamuziki wenzake wa bendi ya Msondo Ngoma wlisema kuwa pengo aliloliacha Mwanamuziki mwenzao TX Moshi William halitazibika kamwe.
Aidha kiongozi wa bendi hiyo Dokta Said Mabera alitamka kuwa Tx Moshi William miongoni mwa nyimbo alizotunga mara baada ya kujiunga na bendi hiyo ni pamoja na Ajuza, Asha Mwanaseif, (aliomtungia mkewe), na wimbo mwingine Ashibaye.
Mabera aliyefanya kazi kwa karibu na TX Moshi William alisema kuwa kama kuna kitu ambacho kilimpa sana heshima kubwa mwanamuziki huyo TX, ni uwezo wake wa kutunga na kuimba, tofauti na wanamuziki walio wengi ambao unaweza kukuta mwanamuziki anajua kuimba lakini hana uwezo wa kutunga nyimbo au ana uwezo wakutunga lakini hana sauti nzuri.
Alisema kuwa mwimbaji huyo alitunga nyimbo nyingi baada ya kuhamia kwenye bendi hiyo lakini alisisitiza kwamba nyimbo zilizotia fora sana ni pamoja na Kilio cha Mtu Mzima, Ndoa Ndoana, Piga Ua Talaka Utatoa, Isihaka Kibene, Kaza Moyo, Harusi ya Kibene, na Ajali.
Wimbo huu Ajali aliutunga akiwa kitandani amelazwa hospitalini kwa matibabu mara baada ya kupata ajali iliyompelekea kuvunjika mguu.
Mara baada ya mwanamuziki huyu kuonekana anapata nafuu, baadhi wapenzi wa bendi hiyo ya Msondo mkoani Tanga, waliomba akakafanyiwe tambiko maalumu ili kipenzi chao TX Moshi William ili apone na kuzidi kuwa na maisha marefu.
TX Moshi William wakati wa uhai wake aliwahi kusema kuwa amepitia katika bendi mbalimbali za muziki ambazo ni pamoja na Safari Trippers, Juwata Jazz, UDA Jazz, na Polisi Jazz, ambayo alipigia kabla kujiunga kundi hilo la Juwata Jazz.
Kufuatia weledi wake katika muziki, nguli huyo alitunukiwa Tuzo mbalimbali za muziki hasa zile zijulikanazo kama Kilimanjaro Music Award.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania vinakariri kuwa Moshi alibatizwa jina la TX, na aliyekuwa mtangazaji wa siku nyingi wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) Julius Nyaisanga.
Nyaisanga alimbatiza jina hilo kutokana na tunzi zake za uhakika. Kwa sasa Nyaisanga ni marehemu.Mwimbajji huyo jina lake hasa ni Shaaban Mhoja Kishiwa, mwenye asili ya Wanyamwezi, ingawa alikuwa akijulikana zaidi kwa jina la TX Moshi William.
Mengi hayafahamiki kwenye maisha yake inagawa wakati fulani TX Moshi William alikaririwa akisema kuwa hali ya kutotulia sehemu moja hasa wakati akiwa mtoto, ilitokana na ugomvi baina ya mama na baba yake.
Ilielezwa kuwa alilelewa na baba yake wa kambo kwa kipindi kirefu cha utoto hadi alipokuwa mtu mzima.
Miongoni mwa wanamuziki ambao tayari wameisha aga dunia na kuacha masikitiko makubwa katika ulimwengu wa muziki wa bendi hiyo ni pamoja na Suleiman Mbwembwe, Mnenge Ramadhani, Muhidin Gurumo, Joseph Maina, Athuman Momba na wengine wengi.
Mbwembwe alikuwa ana sauti ya aina yake na mara nyingi aliimba kwa kupokezana pamoja na Moshi William.Sasa wengi wanahoji nini mstakabali wa bendi hii ya Msondo Music band baada ya kuondokewa na majabari hawa?
Kama alivyotamka Waziri Dewa ambaye ni mratibu wa shughuli za bendi hiyo ya Msondo, itakuwa kazi ngumu na isiyofikiriwa kumpata mwimbaji mwingine mwenye sauti yenye mvuto kama ya TX Moshi William.
Nguli huyo aliacha mjane na watoto watano, wawili wa kike na watatu wa kiume. Wanne wakiwa wa mama mmoja ambao ni Hassan, Maika, Ramadhani na Maada. Jina la mtoto mwingine bado halijafahamika.
Mwanawe Hassan Moshi William amekuwa akijaribu kuvaa viatu vya baba yake, kwa kuimba nyimbo alizokuwa akiimba baba yake, lakini kwa mujibu wa wapenzi wa Msondo Ngoma, wanasema kuwa bado hajamfikia kabisa.
TX Moshi alikuwa ‘chakaramu’ na mbunifu wa kutunga vionjo ikiwemo mtindo ujulikanao wa ‘mambo hadharani’.
Aidha alibuni aina ya ‘Chombezo’ katika nyimbo zao ambapo alipenda kuweka vionjo vyenye kunogesha wimbo. Mfano utasikia "we nani", "kidogo tu..kidogo tu", "kwanini lakini", "watoto wanachezea umeme", "discipline", "fair play" na vingine vingi.
Wakazi wa Keko Machungwa hawawezi kumsahau nguli huyo takriban kila wimbo alikuwa hakosi kuitaja Keko Machungwa, ambako ndiko kulikuwa makazi yake.
Mwisho.
Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0767331200 na 0713331200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...