Afisa mdhibiti ubora wa kiwanda cha CPB Ramadhan Dendegu akionyesha mfumo utakaotumika kiwandani hapo kuhakikisha ubora wa bidhaa itakayokuwa ikizalishwa kiwandani hapo.
Meneja wa kiwanda cha CPB Arusha, Kulwa Rwegasira akielezea ujio wa kiwanda kipya cha CPB kwa lengo la kuwanyanyua wakulima kwa kununua bidhaa zao pamoja na kuzalisha bidhaa bora kwa walaji.
Afisa udhibiti ubora uzalishaji wa kiwanda cha CPB akielezea waandishi wa habari ubora wa mashine za kiwanda hicho katika kudhibiti ubora wa bidhaa zitakazoanza kuzalishwa hivi karibuni. 



Na Seif Mangwangi, Michuzi blog, Arusha 

WAKULIMA wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wanatarajiwa kuondokana na adha ya masoko ya kuuzia mazao yao hususani mahindi na ngano kufuatia kiwanda cha CPB kilichopo jijini hapa kuanza uzalishaji hivi karibuni. 

Akizungumza kiwandani hapo leo, Meneja Mwendeshaji wa kiwanda hicho, Kulwa Rwegasira amesema CPB ambayo zamani ilijulikana kama ‘Monaban’ inatarajia kuanza kununua mazao ya wakulima wa kanda ya Kaskazini na kuzalisha bidhaa mpya ya unga wa dona utakaojulikana kwa jina la ‘Dona bora’.

Kiwanda hicho cha CPB kilichokuwa kikiendeshwa na mwekezaji, hivi sasa kinaendeshwa na Serikali kupitia bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko baada ya Serikali kukichukua kwa kile kinachodaiwa mwekezaji kushindwa kulipa kodi ya pango.

Rwegasira anasema kiwanda hicho kitakuwa kikizalisha aina hizo za unga kwa kutumia vigezo vya ubora wa kimataifa kwa kuwa mbali ya kusambazwa nchini pia utasambazwa kimataifa ikiwemo nchini Kenya. 

Anasema pia kiwanda hicho kiko kwenye matengenezo mbalimbali katika baadhi ya mashine zake ili kiweze kuzalisha unga wa ngano kwaajili ya kutengenezea bidhaa tofauti hususani vitafunwa. 

“Mbali ya kuzalisha dona bora pia tutaanza kuzalisha unga wa ngano ambao na wenyewe utakuwa unga bora tofauti na unga mwingine, lengo letu ni kuhakikisha mwananchi anapata bidhaa yenye ubora wa hali ya juu,”anasema.

Rwegasira anasema CPB pia inatoa huduma za mizani, kusafisha mazao ya wafanyabiashara na wakulima kwa bei nafuu, kukausha mahindi yanayokosa soko kutokana na kuwa na unyevunyevu, pamoja na kukodishia wafanyabiashara maghala ya kuhifadhia mazao.

Kwa upande wao maafisa udhibiti ubora kiwandani hapo Abdallah Dengedu na Jonathan Lunyemela wanasema wamejipanga kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na na bei nafuu ili kuleta tofauti katika soko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...