Wananchi
wa Tanzania upande wa Zanzibar wameendelea kufaidika na mchele
unaotokana na mbegu ya mpunga aina ya SUPA BC iliyoboreshwa kwa
Teknolojia ya Nyuklia kwa kutumia Mionzi aina ya gamma iliyotumika
kununurisha bengu hizo .
Mradi
huo ulifadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) na
kuratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana
na Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa
Kilimo Zanzibar (ZARI) ili kuhakikisha mbegu hiyo inaboreshwa na kuwa
yenye ubora wa hali ya juu.
Akizungumza
katika maonesho ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya maonesho
vya Nyakabindi, Wilayani Bariadi, Mkoani Simiyu, Mtafiti Msaidizi wa
mazao ya kilimo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar Bwana Hamza
Hamid Hamza amesema kuwa mbegu hiyo ina ubora na huzalisha mpunga kwa
wingi na kwa sasa ni chaguo la wakulima na wananchi wengi Kisiwani
Zanzibar.
Amesema
mbegu aina ya SUPA BC, ina uwezo wa kuzalisha mpunga hadi kufikia tani 7
kwa hekta moja ambapo huchukua muda wa siku 130 mpaka kuvunwa kwake
hali ambayo kwa sasa imewahamasisha wakulima wengi kulima aina hiyo ya
mpunga visiwani humo.
“Mchele
unaotokana na mpunga wa mbegu ya SUPA BC ni mzuri, wenye harufu nzuri
na wenye ladha tamu kwa walaji na wakulima wengi wanashawishika kupanda
mbegu hiyo kwa wingi” alisema Hamza Hamid.
Kwa
mujibu wa Hamza amesema kuwa mpunga huo una sifa nyingi ikiwemo urahisi
katika kufikicha tofauti na mbegu nyingine nyingi za mpunga
zilizozoeleka na kuwa mmea wake una urefu wa wastani na usioweza
kuanguka baada ya kubeba mpunga ukiwa shambani hivyo hupelekea kubaki na
mazao yote hadi wakati wa kuvuna pamoja na uwezo wa kutoa machipukizi
mengi wakati wa ukuaji wake.
Mbegu
hiyo ilizinduliwa rasmi na Wizara ya Kilimo na Mifugo ya Zanzibar mwaka
2011 ambapo mpaka sasa inaendelea kulimwa kwa wingi visiwani humo.
Mtaalamu
huyo amesema kuwa teknolojia hii ya nyuklia kwa kutumia mionzi ya Gamma
ikiendelea kutumika inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya
kilimo hasa katika kutafiti wa mbegu mbali mbali za mazao hapa nchini.
Bw.
Hamza pia ameshauri kwamba kwa sasa kutokana na mbegu hiyo ya mpunga
kutumika visiwani Zanzibar pekee , ni wakati muafaka sasa mbegu hiyo
ikaanza pia kutumika pia katika eneo la Tanzania Bara.
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga , Bi Zainab Terak akiwa ameshika mpunga uliotokana
na mbegu ya aina ya Supa BC iliyoboreshwa kwa Teknolojia ya Nyuklia kwa
kutumia mionzi aina ya gamma iliyotumika kununurisha mbegu hizo mradi
ulioofadhiliwa na Shirika la nguvu za Atomiki la kimatifa (IAEA) kwa
kuratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC) kwa kushirikiana
na Chuo kikuu cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa kilimo Zanzibar
(ZARI) .
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...