*Akutwa roud about ya Kawe akiwa hajitambui
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KADA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)ambaye pia amewahi kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro Inocent Shirima amenusurika kufa baada ya kuvamiwa na kukatwa mapanga kichwani akiwa karibu na nyumbani kwake eneo la Goga Kinzugi jijini Dar es Salaam.
Kwa sasa Shirima anaendelea kupata matibabu katika moja ya Hospitali iliyopo jijini Dar es Salaam ili kuokoa maisha yake kutokana na hal yake kutokuwa nzuri kiafya.
Akizungumza na Michuzi Blogu leo Septemba 9,2019 kwa njia ya simu Shirima ameelezea hatua kwa hatua tukio la kuvamiwa kwake a kisha kujeruhiwa kwa kukatawa mapanga kichwani ambapo amesema tukio hilo lilitokea Jumatano ya wiki iliyopita saa tano usiku.
Amesema kuwa akiwa anarejea nyumbani , umbali wa mita 300 kutoka katika nyumba yake kulikuwa na watu wenye bodaboda na mmoja alikuwa amesimama barabarani kama vile anatengeneza bodaboda na alipofika eneo hilo alisimamishwa kama anaombwa msaada.
"Kwa ilikuwa ni maeneo ya karibu na nyumbani sikuwa na wasiwasi, hivyo nikasimamisha gari yangu , baada ya kufungua kioo cha gari nikashtukia nimepigwa na kitambaa usoni.Hiyo ilitokea hata kabla ya kuuliza kuna kitu gani.
"Baada ya hapo inaonekana walichukua gari na kuanza kuzunguka na mimi hadi saa saba usiku.Walinipiga kwa mapanga na nadhani waliamini wameshaniua, hivyo wakaenda kunitelekeza katika eneo la round about ya barabara ya Kawe.Lengo lao ilikuwa ni kuniweka hapo ili nigogwe na gari itakayopita,"amesema Shirima.
Ameongeza kuwa wakati wanafanya hayo yote hakuwa anajitambua kwani alishapoteza fahamu na ndio maana waliokuwa wanafanya unyama huo waliamini ameshakufa."Wamenikata mapanga, wakaniburuza kwenye lami na kisha kunitelekeza nije nigongwe na gari."
Amefafanua kuwa baada ya kumjeruhi na kumuacha eneo hilo, watu hao wamechukua fedha zake Sh.milioni 11 ambazo alichelewa kuzipeleka katika duka la saruji kwani anajihusisha na biashara ya kuuza tofali.Pia wamechukua flashi mbili,simu ya mkononi la laptop.
Hata hivyo amesema kuwa baada ya kutupwa eneo hilo, kuna vijana wengine wa bodaboda wa maeneo ya nyumbani kwake baada ya kumuona akiwa hapo walisimamisha bodaboda zao kwa ajili ya kumpa msaada na hata wao walikuwa wanajua ameshakufa.
"Walidhani ni maiti na baada ya kuniona napumua ndipo waliponchukua na kunipeleka Hospitali ya Kairuki ambapo pale nilifanyiwa opereshani kwa saaa nane,"amesema Shirima.
Alipoulizwa kwa sasa hali yake ikoje ?Amejibu hali yake bado mbaya na kuna eneo ambalo amehifadhiwa akiendelea kupata matibabu.Hata hivyo amesema kwa kuwa yeye ni mwanasiasa kuna maswali mengi anajiuliza katika tukio hilo.
"Kama ni majambazi walishanidhibiti na nikawa sijitambui kwanini watake kuniua kwa kunikata mapanga kichwani?Ndani ya gari kulikuwa na vitu muhimu zaidi wameacha, kulikuwa na nyaraka muhimu hawakuchukua, kwanini? Hili tukio linaleta wakati mgumu kwangu na familia yangu ambayo kwa sasa haina amani kabisa,"amesema Shirima.
Amesema kama lengo lao ni kumuua maana yake wataendelea kumtafuta tena kwani walichotarajia sicho ambacho kimetokea."Waliamini wameniua , lakini niko hai unadhani nini ambacho kitaendelea?"
Alipoulizwa kama tayari Polisi wanafahamu tukio hilo, Shirima amejibu Polisi wanazo taarifa na amesikia wanaendelea na uchunguzi lakini yeye kama yeye bado hajahojiwa na polisi kuhusu tukio hilo ikiwa pamona na kuchukua maelezo yake.
Alipoulizwa anahisi nini kutokana na tukio hilo, amejibu hana jibu la moja kwa moja lakini kwa kuwa yeye ni mwanasiasa huenda ndani yake imeingia siasa
"Tukio hili lina mambo mengi, katika uchaguzi uliopita niligombea ubunge na kushika nafasi ya pili.Nakumbuka wakati wa uchaguzi kule nyumbani Moshi watu walivamia nyumba yangu, walimkuta baba yangu mdogo ambaye walimuua kwa kumchinja,"amesema Shirima.
Amesema anakumbuka siku hiyo alipanga kusafiri lakini alibadili safari , hivyo waliovamia nyumba yake waliamini yupo lakini baada ya kufika wakamkuta baba yake mdogo na ndipo walipoamua kumuua.
"Mawazo yangu nahisi hili tukio lina siasa na sasa tunakwenda kwenye uchaguzi sijui nini kitatokea tena.Siamini katika ujambazi maana kama ni majambazi walishanidhibiti iweje wanipige mapanga,"amesisitiza Shirima.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...