Charles James, Michuzi TV
TIMU za Soka za Dodoma Jiji FC na Singida United zimetoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa kirafiki uliopigwa katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma.
Dodoma FC inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza ndio waliokua wenyeji wa mchezo huo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujiweka fiti na msimu mpya wa daraja la kwanza utakaoanza kutimua vumbi Septemba 14 ya mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Timu hiyo, Mbwana Makata amesema mchezo wa leo ni muendelezo wa michezo ya kirafiki ambayo wamekua wakiicheza kwa ajili ya kujiimarisha kabla Ligi hiyo haijaanza.
Amesema kitendo cha Timu yake kucheza michezo minne ya kirafiki na Timu za Ligi Kuu kimewapa mwanga wa wapi ambao wanapaswa kurekebisha kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
" Ni kweli suala la ufungaji limekua changamoto kwenye michezo yetu ya kirafiki lakini mabadiliko yamekuepo kuanzia mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City hadi huu wa Singida.
" Tunaamini tumeimarika na tutafanyia kazi mapungufu machache kabla ya kuanza kwa msimu mpya. Ombi letu kwa wanadodoma ni wao kuendelea kutuunga mkono na sisi tunawaahidi hatutowaangusha," amesema Makata.
Nae Kocha wa Singida United, Fred Minziro amekipongeza kikosi cha Dodoma FC kwa kiwango walichoonesha na kusema kama kocha Makata atafanyia mapungufu machache yaliyoonekana basi watakua na Timu bora itakayoweza kuhimili mikikimikiki.
" Tunashukuru Mungu mchezo wetu na Dodoma FC umemalizika salama. Timu Zote mbili zimekua na changamoto za ufungaji lakini naamini tutafanyia kazi kabla ya mchezo wetu wa pili dhidi ya Namungo utakaochezwa Septemba 14.
" Kwa upande wa Dodoma FC Niwapongeze wana kikosi chenye wachezaji wazuri na wazoefu. Pia wana kocha makini na mwenye kujua Ligi Daraja la kwanza. Wakifanyia kazi mapungufu kwenye eneo la ushambuliaji nawaona kabisa wakipanda Ligi kuu," amesema Minziro.
Kikosi cha Dodoma Jiji FC kinachojiandaa na Ligi Daraja la kwanza itakayoanza kutimua vumbi Septemba 14 mwaka huu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...