Jumuiya ya wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya juu Nchini Tanzania (TAHLISO) limeunga mkono agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuboreshaji mitaala yake ya ufundishaji ili kuwapa fursa kuingia katika ajira binafsi hususani ujasiriamali.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam , Mwenyekiti wa TAHLISO Peter Niboye alisema kimsingi suala hilo ni muhimu kwa kuwa litasaidia kuwaondoa maelfu ya vijana waliopo mitaani ambao wamekosa ajira licha ya kuwa na ufaulu mzuri katika masomo yao vyuoni.
Awali akifungua kongamano la kitaifa la ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa agizo kwa taasisi za elimu kuboresha mitaala yake ili kuwasaidia vijana kuweza kujiajiri.
Akizungumzia hatua hiyo Niboye alisema agizo la Waziri Mkuu lina umuhimu mkubwa wakati huu ambao Tanzania inatekeleza sera yake ya uchumi wa viwanda huku akiitaka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kulisimamia suala hilo ili utekelezaji wake uweze kufanyika haraka iwezekanavyo.
“Hii siyo mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu kuligusia suala hili, alifanya hivyo pia Agosti 10 alipokuwa akifungua mkutano wetu wa kwanza mara baada ya hotuba yetu kuligusia suala hilo, kimsingi ifike mahali Wizara ya elimu ilisimamie suala hili ili kuwapa fursa vijana ya kujiajiri” alisema Niboye.
Aidha alisema uwepo wa mitaala mizuri inayoweza kumuandaa mhitimu kujiajiri katika soko la ajira, kwa sasa lina umuhimu wa kipekee ikizingatia kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza sera yake ya uchumi wa viwanda iliyowezesha vijana wengi kuona umuhimu wa kupata elimu inayoweza kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya viwanda.
“Hata ukitazama katika vyuo mbalimbali hivi sasa utagundua kuwa vijana wengi wamekuwa wabunifu kwa kubuni mitambo inayoweza kuzalisha bidhaa mbalimbali, hii ni fursa ambayo kama Wizara ya elimu itaweza kuisimamia kikamilifi tutaweza kupiga hatua kimaendeleo” aliongeza Niboye.
Aidha akizungumza katika kongamano hilo,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema sekta za elimu nchini inatakiwa kuandaa sera, sheria,kanuni na taratibu ambazo zitawawezesha watanzania kushiriki katikautekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini.
Alisema umefika wakati wakati kwa taasisi au sekta ya elimu kubadilisha mitaala ya shule ili kuwawezesha vijana kuingia katika shughuli za ujasiriamali badala ya mitaala ya sasa ambayo haitoi fursa hiyo.
Mwenykiti wa TAHLISO,Peter Niboye akizungumza na waandishi wa habari( hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaa kuhusu kuunga mkono agizo la Waziri Mkuu kuhusu taasisi za elimu kuboresha mitaala.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...