Na Raya Hamad –WKS
Mashirikiano ya pamoja kutoka kwa wanufaika wa huduma ya msaada wa kisheria na watoaji huduma hio ndio chachu itakayopelekea utekelezaji mzuri wa majukumu ya Idara ya Msaada wa Kisheria katika kuleta ufanisi wa majukumu ya kazi zao
Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria Bi Hanifa Ramadhan Said ameyasema hayo kwenye mkutano uliowashirikisha baadhi ya wanufaika wa msaada wa kisheria uliofanyika katika ukumbi wa mkutano Wizara ya Katiba na Sheria Mazizini
Bi Hanifa amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanzisha Idara ya Msaada wa Kisheria ili kuratibu utoaji na upatikanaji wa huduma ya kisheria kwa wananchi wote bila ya kujali uwezo wa kifedha kwa mtaka huduma
Aidha Bi Hanifa amewashukuru wanufaika hao waliopatiwa msaada kutoka vituo vinavyotoa huduma za msaada wa sheria kwa kukubali kufuata taratibu na kutoa mashirikiano pale wanaposhughulikiwa malalamiko yao jambo ambalo linarahisisha kupata haki zao stahiki kwa muda muafaka
Pia ametoa pongezi za dhati kwa watoaji wa huduma ya msaada wa Kisheria kwa kuwapokea na kuwashughulikia matatizo yao wananchi bila upendeleo jambo ambalo limepelekea kutokuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wanufaika waliofika katika vituo vyao
“nimefarijika na michango iliyotolewa leo hii kutoka kwenu hakuna hata mmoja aliyelalamika kuwa hakutendewa haki wakati alipotaka huduma ya msaada wa Kisheria na mmeona mafanikio yake hivyo msisite kuwafahamisha na wengine pale wanapopata matatizo hasa wanapodai haki zao za msingi wasiyamalize kienyeji au kuona muhali bali wafuate taratibu vituo hivi vipo kwa ajili yenu”alisisitiza
Hata hivyo ameomba kutosita kutoa maoni ama ushauri kwa Idara ya Msaada wa Kisheria ili kuenda sambamba na kasi ya maendeleo kwani lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kukuza ustawi wa wananchi wake katika nyanja zote za maisha kwa kuwahudumia na kuwaletea maendeleo na kuwaondolea uzito wa maisha yao ya kila siku
Bi Hanifa ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweza kufanikisha kupatikana Sera, Sheria na Kanuni inayosimamia sekta nzima ya msaada wa kisheria
Wakitoa mada kuhusu huduma za msaada wa kisheria watoa mada na uchambuzi wa vifungu vya kanuni katika mafunzo hayo wanasheria ndugu Amour Omar Mbwana na ndugu Omar Haji Gora wamesema huduma za msaada wa Kisheria zinajumuisha ushauri wa kisheria, uwakilishi mahakamani au katika mabaraza, kutoa elimu ya kisheria, pamoja na kutayarisha nyaraka za kisheria na taarifa kuhusiana na mambo ya kisheria
Aidha wamefafanua baadhi ya vifungu kwa watu wasiokuwa na sifa ya kupatiwa msaada wa kisheria kuwa ni pamoja na kampuni, shirika, taasisi ya umma, Jumuiya ya kiraia , Jumuiya isiyokuwa ya kiserikali au mtu mwengine wa kisheria .
Msisitizo pia umewekwa kuwa watoaji wa msaada wa kisheria hawatatoa huduma za msaada wa kisheria kuhusiana na kesi za madai zikiwemo masuala yanayohusu ulipaji wa kodi, ulipaji wa madeni na katika kesi za ufilisi na kutoweza kulipa madeni
Nao washiriki wa mafunzo hayo wametoa shukurani zao kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuanzisha Idara ya Msaada wa Kisheria na kuomba idara hio kuendelea kutoa elimu na kuielimisha jamii ili waweze kuifahamu na kuona umuhimu wa kufikisha malalamiko yao pale wanapohitaji usaidizi wa huduma ya msaada wa kisheria
Washiriki hao wamezungumzia kuwa utaratibu huo wa kuwasaidia kisheria wananchi wasiokuwa na uwezo Serikali inastahili kupongezwa kwa sababu wamo wananchi wengi wanyonge wenye vilio vya muda mrefu, lakini hawana pa kuvipeleka kutokana na unyonge.
A
Wameeleza kuwa jambo la muhimu kwa Taasisi inayohusika na Utoaji wa Huduma za msaada wa Kisheria kuhakikisha wasiokuwa na uwezo ndio wanaonufaika na utaratibu huo na kuomba kufanywa kila liwezekanalo kuwazuia wale wenye uwezo wa kujisimamia ama kuendesha kesi ili waweze kupata haki zao wenyewe kutojingia katika utaratibu huo na kuwazuia walengwa.
Wamesema kwamba wamo wananchi wengi ambao uwezo wao na mwamamko wa kupigania haki zao ni mdogo, huku baadhi ya wananchi hao wanashindwa na hata nauli ya kuwawezesha kufika mahakamani, hivyo uamuzi huo ni jambo la kupongezwa kwa sababu umelenga hasa kuwakomboa wenye mahitaji.
Mkurugenzi Idara ya Mswaada wa Kisheria Zanzibar Bi Hanifa Ramadhan Said akifungua mafunzo kwa wanufaika wa huduma ya Mswaada wa Kisheria kutoka Taasisi tofauti
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...