Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv.
WATU sita wakazi wa Jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kukutwa na meno 413 ya tembo na meno mawili ya kiboko yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni nne.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amewataja wawhitakiwa haoni kuwa ni, Hassan Likwena maarufu Nyoni (39) na ndugu yake, Bushiri Likwena, Oliver Mchuwa (35), Salama Mshamu (21), Hidary Sharifu maarufu White (44) na Joyce Thomas (33).
Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo kuwa kati ya Januari Mosi, 2017 na Septemba 3, 2019 katika maeneo tofauti ya Mtwara, Pwani na Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walishiriki genge la uhalifu.
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kupokea vipande 413 vya meno ya tembo vyenye thamani ya USD 1,755,000 pamoja na vipande vya meno ya kiboko mawili yenye thamani ya USD 1,500 vyote vikiwa na thamani ya Sh 4,043,463,000 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Imeendelea kudaiwa kuwa, Septemba 3, mwaka huu maeneo ya Saku Chamazi wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walikutwa na vipande hivyo vya meno ya tembo bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shtaka la tatu, Wakili wa Serikali, Salum Msemo alidai tarehe na maeneo hayo, washitakiwa walikutwa na vipande viwili vya meno ya kiboko yenye thamani ya USD 1,500 sawa na Sh 3,453,000.
Pia imedaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, 2017 na Septemba 3, mwaka huu washitakiwa walikutwa na vipande 413 vya meno ya tembo na vipande viwili vya meno ya kiboko vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni nne wakati wakijua kwamba kitendo hicho ni kiashiria cha kosa la uwindaji haramu.
Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchimu hadi Mahakama Kuu au pale watakapopatiwa kibali kutoka kwa DPP. Kwa mujibu wa upande wa mashitaka upelelzi katika shauri hilo bado haujakamilika na waliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. kesi hiyo imeahirishwa hadi hadi Oktoba Mosi mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...