Na Ripota Wetu,
BENKI ya KCB Tanzania kupitia KCB Biashara Club imewapeleka wafanyabiashara 10 kwenda nchini China kwa lengo la kukutana na wazalishaji halisi wa bidhaa mbalimbali ili kujifunza 
na kutafuta namna bora ya kuweza kuboresha biashara zao. 

Wafanyabiashara hao watakaa nchini China kwa siku 10 na kupata fursa ya kutembelea miji miwili mikubwa. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Mahusiano na Mawasiliano wa benki ya KCB, Christina Manyenye alisema  wameanza kuwapeleka China wafanyabiashara hao ambao ni wateja wa benki hiyo ili wakakutane na wazalishaji halisi na si walanguzi au madalali ambao uwauzia bidhaa kwa 
bei ya juu. 

Alisema kwa muda mrefu wafanyabiashara nchini ambao wanakwenda China 
wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo za lugha na kuuziwa vitu bei za juu hivyo kupitia safari hizo wanazoziandaa mambo hayo hayatajitokeza. 

“Tatizo kubwa ambalo wafanyabiashara walikuwa wanakutana nalo ni kuuziwa vitu kwa bei  ya juu na walanguzi au madalali sasa kupitia safari hii tutawakutanisha na wale wazalishaji halisi ambao wanaviwanda ambapo watapata fursa ya kutembelea viwanda vyao kisha kutoa oda za kutengenezewa bidhaa zao. 

Pia kuna tatizo la lugha kule, kupitia safari hii tuliyoiratibu sisi KCB Benki 
tutawapatia wakalimani ambao watatembea nao kila mahali ili kurahisisha mawasiliano yao na wazalishaji hao,” alisema. 

Kwa upande wake  Meneja Uhusiano wa Wateja Wadogo na wa Kati wa benki hiyo, Moses Kisaka alisema wanamatumaini kwamba siku hizo 10 wafanyabiashara hao wataweza kuzunguka na 
kukutana na wazalishaji pamoja na kutumia fursa hizo kufanya manunuzi ya bidhaa zao. 

Alisema wafanyabishara hao watakutana na wazalishaji halisi watakaowauzia vitu kwa bei  ya chini kuliko ilivyokuwa awali walipokuwa wakienda wenyewe na kukutana na walanguzi  waliokuwa wanawauzia vitu kwa bei ya juu. 

“Tunafanya hivi kwa lengo la kuwasaidia wapunguze gharama za kupata bidhaa, tunaamini safari hizi zitakuwa ni muendelezo na tunatumaini mwakani kuwapeleka wafanyabiashara 
wengi zaidi,” alisema. 

Aidha alisema benki hiyo imeanzisha kitengo cha KCB Biashara Club 
kwa lengo la kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara mbalimbali na kuzungumza juu ya changamoto na fursa za kibiashara wanazokutana nazo. 

Kwa upande wake Mwakilishi wa wafanyabiashara wanaoenda China, Saada Sipemba alisema safari hiyo itawasaidia kupata fursa ya kuona maonyesho makubwa yanayofanywa na wenye viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo vyombo vya ndani pamoja na 
mashine.

“Pia itatuwezesha kwenda kujifunza na kukutana na wazalishaji wenyewe bila  kupitia kwa madalali wowote hivyo itatusaidia kununua bidhaa kwa bei nafuu na kuja kuziuza nchini kwa bei nafuu pia,” alisema Sipemba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...